1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Annan alaani mauaji ya mjumbe wa Papa

30 Desemba 2003
https://p.dw.com/p/CFnq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi ANNAN amekosoa na kulaani mauaji ya mwakilishi maalum wa Papa YOHANA PAULO wa 2 nchini Burundi akiyataja kuwa ya kikatili. Askofu Michael COURTNEY, ambae ni mwenye asili ya Ireland alifariki dunia hospitalini baada ya kujeruhiwa jumatatu katika shambulio la bunduki kusini mwa mji mkuu wa Burundi, Bujumbura. Msemaji wa Bwana ANNAN, Fred ECKHARD amemkariri Katibu Mkuu akimsifu mwakilishi huyo wa Kanisa kwa mchango wake mkubwa aliyotoa katika juhudi za amani ya Burundi. Kauli kama hiyo imetolewa pia na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland, Bertie AHERN na Kadinal wa mjini Dublin Desmond CONNELL, wakitaja kufadhaishwa na mauaji hayo ya Askofu COURTNEY. Mjumbe huyo wa Kanisa, 58, aliwasili Bujumbura Agosti 2000 na kutarajiwa kumaliza uwakilishi wake mwezi Januari 2004. Jeshi la serikali ya Burundi limedai kuwa mauaji yake yamefanywa na waasi wa Palipehutu-FNL katika eneo la Minago, kusini mwa nchi hiyo. Waasi hao, ambao ndio kikundi pekee cha wapiganaji kinachoendelea kukaidi mazungumzo ya amani na jeshi, wamekana kuhusika katika tukio hilo. Kabla ya kwenda Burundi, askofu COURTNEY alikuwa mwakilishi wa Papa YOHANA PAULO kwenye makao makuu ya Bunge la Ulaya mjini Strasburg.