1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW DELHI:Mafuriko yaua watu 50 India na Bangladesh.

21 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEYu

Kiasi cha watu 50 wamekufa na wengine kwa mamia hawajulikani walipo,baada ya tufani kubwa kukumba maeneo ya kusini mwa India na Bangladesh katika Ghuba ya Bengal.

Maofisa wa serikali ya India wamesema kiasi cha watu 100,000 wameachwa bila makazi,baada ya nyumba zao kuzolewa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa wiki hii,katika wilaya za pwani jimboni Andhra Pradesh.

Wengi wa waliokufa nchini India ama walinaswa na umeme ama walikufa baada ya kuangukiwa na kuta za nyumba.

Wafanyakazi wa vikosi vya uokoaji wanawahamisha wale waliokwama na helikopta za jeshi zinadondosha vyakula na chupa za maji kwa watu waliozingirwa na maji na pia zinawaondosha watu ambao wamesalimisha maisha yao katika mapaa ya nyumba.

Katika nchi jirani ya Bangladesh,wawakilishi wa jumuia ya wavuvi,wamesema mamia ya wavuvi hawajulikani walipo.Wamesema mitumbwi mingi iliyokuwa na wavuvi hao ilizama wakati wa tufani hiyo.