1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu asifu uhusiano wa Israel na India

15 Januari 2018

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameisifu "enzi mpya" katika mahusiano kati ya nchi yake na India, wakati aliposaini mikataba kadhaa na mwenyeji wake siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/2qs96
Indien - Modi und Netanyahu in Neu Delhi
Picha: IANS/MEA

Hii ni ziara ya kwanza kuwahi kufanywa na Waziri Mkuu wa Israel nchini India katika kipindi cha miaka 15.

"Huu ni mwanzo wa enzi mpya katika urafiki mkubwa kati ya India na Israel. Ulianza na ziara ya kihistoria ya Waziri Mkuu Modi nchini Israel ambayo iliweka matumaini makubwa. ninaendelea na ziara yangu hapa," alisema Netanyahu, "ambayo lazima niseme inanipa hisia kubwa pamoja na mke wangu na watu wote wa Israel na nadhani ni ishara ya ushirikiano wetu mzuri wa kuleta ustawi na amani na maendeleo kwa watu wetu." aliongeza Netanyahu.

Narendra Modi, aliweka historia mnamo mwezi Julai wakati alipokuwa kiongozi wa kwanza wa INDIA kuwahi kuitembelea Israel.

Nchi hizo zinapanga kuimarisha ushirikiano

Modi alisema mazungumzo yao yaliangazia ulinzi, biashara na mikakati ya kupambana na ugaidi, pamoja na maeneo mapya ya ushirikiano ili kuutanua ushirika wao.

Indien -  Modi und Netanyahu in Neu Delhi
Netanyahu na Modi wakiweka shada la maua New DelhiPicha: IANS/MEA

"Rafiki yangu, karibu India. Ziara yako, Waziri Mkuu, ni tukio lililosubiriwa kwa muda mrefu katika safari ya urafiki wetu kati ya India na Israel. Ziara yako pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya India na Israel," alisema Modi.

Modi ameongeza kuwa nchi hizo mbili zinapanga kuimarisha ushirikiano wao kwa ajili ya kuyagusa maisha ya watu, kama vile kilimo, sayansi na teknolojia na usalama.

Israel na India zilisaini mikataba tisa katika maeneo ya mafuta na gesi, nishati jadidifu, ulinzi, usafiri wa angani, usalaam wa mitandao ya intaneti, ushirikiano wa sekta ya filamu na uwekezaji.

Mahusiano kati ya nchi hizo yamekuwa mazuri

Netanyahu ambaye aliandamana na ujumbe mkubwa wa kibiashara, atahudhuria baadaye Jumatatu mkutano wa kilele wa pamoja wa kibiashara na mafaisa wakuu watendaji nchini India.

Premierminister Indien Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: Getty Images/AFP/P. Singh

India ina mahusiano ya muda mrefu na ulimwengu wa Kiarabu na imeunga mkono juhudi za Palestina kwa miongo mingi. Nchi hiyo ilianzisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel mnamo mwaka wa 1992.

Mahusiano kati yao yamekuwa mazuri tangu wakati huo, huku Israel ikiwa muuzaji mkubwa wa vifaa vya ulinzi nchini India.

Mapema Jumatatu, kiongozi huyo wa Israel alipewa mapokezi ya heshima katika kasri la rais na kisha baadaye akatembelea eneo la kumbukumbu la Mahatma Gandhi, kiongozi wa vuguvugu la uhuru wa India.

Mwandishi: Bruce Amani/DPAE
Mhariri:Yusuf Saumu