1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nelson Mandela atoa hotuba yake kwenye mkutano wa Bangkok.

Josephat Charo15 Julai 2004

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela amesema katika mkutano kuhusu ukimwi unaoendelea mjini Bangkok, kwamba ni baraka kuona ulimwengu wote ukiungana pamoja katika jitahidi za kupambana na ugonjwa hatari wa ukimwi.

https://p.dw.com/p/CEHv
Nelson Mandela akizungumza kwenye mkutano wa Bangkok.
Nelson Mandela akizungumza kwenye mkutano wa Bangkok.Picha: AP

Nelson Mandela ameelezea wasiwasi wake kwamba ikiwa ugonjwa wa kifua kikuu ambao huwaua wagonjwa wengi wa ukimwi utapuuzwa, basi huenda ulimwengu ukashindwa katika vita dhidi ya ukimwi.

Kadri watu milioni 14 wanaugua ukimwi na kifua kikuu duniani kote. Asilimia 70 kati yao wanaishi Afrika, bara ambalo limeathiriwa vibaya zaidi na ugonjwa wa ukimwi ambao tayari umewaua watu milioni 20 ulimwenguni kote.

Virusi ambavyo husababisha ukimwi, hupunguza kinga mwilini na kuufanya mwili kuwa dhaifu usiweze kupambana na magonjwa kama vile kifua kikuu. Ugonjwa wa kifua kikuu umewaua kadri thuluthi moja ya watu ambao wameaga dunia kwa sababu ya ukimwi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Nelson Mandela alieleza vile yeye mwenyewe alivyopambana na ugonjwa wa kifua kikuu alipokuwa gerezani kwa miaka 27 kwa kupinga maongozi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Aidha, alisema kuugua ugonjwa huu ni kama kuhukumiwa kunyongwa na akahimiza ulimwengu kuongeza jitihada zaidi katika kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu ambao huua watu kadri milioni mbili kila mwaka.

Harakati za kuvumbua dawa ya ukimwi na kifua kikuu zilipata udhamini mpya wa dola milioni 45 kutoka kwa kampuni ya Bill Gates. Pesa hizi zitatumika katika kusaidia kutafuta mbinu za kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu na ukimwi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi. Utafiti huu unanuiwa kufanyika Afrika na Marekani Kusini kwa mda wa miaka saba.

Mandela, atakayefikia umri wa miaka 86 juma lijalo, ameendelea kufanya kampeni dhidi ya ukimwi kwa bidii kubwa. Tayari ameweza kuchangisha mamilioni ya dola katika shirika lake la Nelson Mandela Foundation linalopambana na ukimwi. Afrika Kusini ndilo taifa liloathiriwa vibaya zaidi na janga la ukimwi ulimwenguni kote.

Habari zaidi zinasema kwamba wawakilishi wa vijana katika mkutano huo wa Bangkok wamesema kampeni nyingi za kuwahamasisha vijana juu ya ukimwi hazifaulu kwa sababu hazizingatii mambo ya kufanya mapenzi. Wamewalaumu wafanyakazi wa afya kwa kutowashughulikia vijana kikamilifu, jambo ambalo limewafanya wengi wao kutopimwa ili kujua kama wana virusi vya ukimwi.

Kuwafundisha vijana kuhusu ukimwi ni jambo la dharura hasa ingizingatiwa kwamba zaidi ya nusu ya watu milioni 5 walioambukizwa ukimwi walikuwa vijana. Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa limesema kati ya vijana elfu 5 na elfu 6 huambukizwa virusi vya ukimwi kila siku duniani kote. Thuluthi moja ya watu milioni 38 wanaougua ukimwi ni watu kati ya umri wa miaka 15 hadi 24, wengi kati yao wakitoka Afrika.

Raoul Frasen, kijana anayeugua ukimwi kutoka Uholanzi amesema kwamba vijana sasa wamechoshwa na kampeni kuhusu ukimwi ambazo hazizingatii maisha yalivyo hivi sasa. Akizungumza kwenye mkutano huo, Fransen alisema mitindo inayotumika ili kuwahamasisha vijana imepitwa na wakati, hivyo hakuna anayetaka kuhudhuria kampeni hizo. Aliilaumu Marekani kwa kusisitiza kuwa watu wajizuie kufanya mapenzi kama njia ya hakika ya kujikinga na ukimwi. Alisema vijana wanatakiwa kufunzwa maana ya kufanya mapenzi, raha na athari zake.

Ijapokuwa ukimwi umeendelea kuhatarisha maisha ya binadamu kwa miongo mitatu sasa, watu bado wanaogopa kuzungumza waziwazi na vijana kuhusu jambo la kufanya mapenzi kiholela. Ikiwa vijana hawataelezwa wazi ni vipi mtu anaweza kuambukizwa ukimwi, itakuwa vigumu kuyaokoa maisha yao kwani hao hutaka tu kuonja asali wasijue kuna sumu kali ndani yake.

Barani Afrika ni kama mwiko kuzungumza na mtoto wako juu ya mambo ya kufanya mapenzi. Ni vigumu sana kwa kijana kupata ufahamu wa mambo haya yeye mwenyewe pasipo kuelekezwa. Hivyo basi vijana wengi huambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ugonjwa hatari wa ukimwi.