1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kimaskini zapata kijisauti zaidi katika Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.

Mohamed Dahman30 Aprili 2008

Nchi za kimaskini zimepatiwa sauti kidogo katika Shirika la Fedha la Kimataifa IMF ingawa hatua hiyo bado inaonekana kuwa ni ndogo lakini ni kubwa kabisa kuwahi kuchukuliwa katika kipindi cha miaka 60.

https://p.dw.com/p/Dr15
Mikutano ya Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Benki ya Dunia mara nyingi hukabiliwa na maandamano ya kuipinga kama ilivyotokea mjini Prague Jamhuri ya Czeck mwezi wa Septemba 2000.Picha: AP
Mataifa ya kitajiri hadi sasa yamekuwa na asilimia 60.5 ya haki ya kupiga kura katika shirika la Fedha la Kimataifa IMF.Mageuzi yaliopitishwa mapema wiki hii yalipunguza haki yao hiyo hadi kuwa asilimia 57.93.

Kwa nchi nyingi zinazoendelea na mashirika yasio ya kiserikali NGOs hatua hiyo haitoshi lakini ni badiliko moja kubwa kabisa katika haki ya kupiga kura kwa kuyapendelea mataifa yanayoendelea katika shirika hilo la IMF ambalo limeundwa hapo mwaka 1946.

Nchi wanachama wa shirika hilo zilikuwa zimepewa muda hadi tarehe 28 mwezi wa April kuidhinisha pendekezo la kuzipa nchi zinazoendelea nguvu zaidi ya usemi katika taasisi hiyo.

Shirika la habari la IPS limeelezwa kwamba pendekezo hilo limeidhinishwa kwa asilimia 92.93 ya kura ikiwa ni zaidi ya asilimia 85 kiwango cha chini kinachohitajika ili kuwezesha kitengo kipya cha haki ya kupiga kura kuanza kutumika.

Nchi wanachama mashuhuri wa IMF kama vile Urusi na Saudi Arabia zilipiga kura kupinga pendekezo hilo kwa sababu uzito wao wa kupiga kura unapunguzwa.Lakini kupinga kwao huko hakukuwa na nguvu za kutosha kuzuwiya kupitishwa kwa uamuzi huo.

Nchi zinazoendelea zimekuwa zikilalamika kwa miaka mingi kwamba hazina usemi wa kutosha ndani ya shirika hilo la fedha la kimataifa.Nyingi ya nchi hizo pia haziamini kwamba mfuko huo wa fedha kwa ukweli uko kwa maslahi yao.Kwa sababu hiyo baadhi ya nchi zinazoendelea zimejilimbikizia akiba kubwa sana ya fedha ili kuhakikisha kwamba hawatoihitaji tena IMF pale kutakapotokea matatizo ya kifedha.

Msaada wa IMF kwa nchi nyingi zilizokuwa na shida huko nyuma umekuwa ukitolewa kwa masharti ambayo umekuja kusababisha madhara ya muda mrefu kwa afweni ya muda mfupi.Lilo tata kabisa miongoni mwa masharti hayo ni Mpango wa Marekebisho ya Kiuchumi ambao IMF ilikuwa ikidai utekelzwe ili nchi ziweze kupatiwa misaada.

Mpango huo wa marekebisho ya kiuchumi ulikuwa ukitaka kupunguzwa kwa vikwazo vya kuingiza bidhaa kwenye nchi na hatua ya kuelekea kile kinachoonekana kuwa uchumi huru unaotegemea nguvu za masoko ambako mara kwa mara kumekuwa kukiathiri viwanda vya ndani ya nchi hizo na bidhaa zao.Kwa kawaida mageuzi hayo yalikuwa yakitajwa kama ni Muafaka wa Washington ambapo kwa sasa kuna machache ya muafaka huo.

Uwezo wa ushawishi unaongezeka wa nchi zinazoendelea dhidi ya masharti hayo na kuongezeka kwa nguvu za uchumi wao kumezidisha shinikizo kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kufanya mageuzi.Hapo mwaka 2006 haki za kupiga kura za Korea Kusini,Mexico,China na Uturuki ziliongezwa. Wiki hii hatua muhimu ya pili imeidhinishwa.

Kundi la nchi zinazoendelea hivi sasa limeona fungu lao la haki ya kupiga kura limeongezeka kutoka asilimia 31.7 hadi kufikia asilimia 34.49.Sehemu kubwa ya ongezeko hilo limekwenda kwenye nchi zinazoinukia kiuchumi.

Nchi kama Brazil,China na India zimepata nguvu zaidi ya kupiga kura.

Nchi wanachama zenye ushawishi mkubwa za IMF zinaendelea kuwa Marekani , Japani,Ujerumani na kundi linaloongozwa na Ubelgiji linalojumuisha Uturuki,Austria na nchi kadhaa za Ulaya ya Kati na Mashariki.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo la Fedha la Kimataifa daima amekuwa akitokea katika nchi ya Ulaya kutokana na makubaliano miongoni mwa nchi zinazoendelea.