1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Napoli yatwaa taji la Coppa Italia.

Deo Kaji Makomba
18 Juni 2020

Huko nchini Italia timu ya soka ya Napoli iliifungasha virago timu ya Juventus kwa kuitandika mikwaju 4-2 ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika mchezo wa fainali ya kuwania kombe la Coppa Italia

https://p.dw.com/p/3e0QD
Copa Italia Juventus Turin - SSC Neapel
Wachezaji wa Napoli wakishangilia kutwaa taji la Coppa ItaliaPicha: Reuters/A. Lingria

Huko nchini Italia timu ya soka ya Napoli iliifungasha virago timu ya Juventus Turin kwa kuitandika mikwaju 4-2 ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika mchezo wa fainali ya kuwania kombe la Coppa Italia, fainali iliyopigwa Jumatano tarehe(17.06.2020) na kumfanya kocha wa timu hiyo Gennaro Gattuso, kutwaa taji lake la kwanza kubwa tangu kuanza kushika mikoba ya ualimu wa kandanda.

Wachezaji Paulo Dybala na Danilo, waliikosesha juhudi za kwanza za Juve kwenye upigaji wa penaiti wakati Napoli ilipobadilisha majaribio yake yote ya kushinda kombe hilo kwa mara ya sita na kumaliza matumaini ya Juve ya kupata mataji matatu katika msimu huu.

Ilikuwa ni taji la kwanza kutwaliwa katika msimu huu wa soka nchini Italia ambao umeanza tena mara baada ya kupigwa marufuku mikusanyiko ya watu na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo michezo kufuatia kutokea kwa mripuko wa janga la virusi vya Corona.

Ingawa ilikuwa imepangwa kwa wachezaji kukusanya medali zao katika hafla yao, wachezaji wa napoli medali zao walizipata kupitia kwa marais wa klabu hiyo, Aurelio De Laurentiis na Andrea Agnelli.

Ushindi huo wa Napoli imekuwa ni mafanikio mazuri kwa kocha Gattuso mwenye umri wa miaka 42 aliyechukua mikoba ya kuifundisha Napoli mnamo Desemba mwaka jana na timu hiyo kujitenga baada ya wachezaji hao kuasi dhidi ya kambi ya mazoezi iliyowekwa na De Laurentiis.

 Reuters