Mzozo wa Korea ya Kaskazini na Marekani wazidi makali
14 Aprili 2017Onyo la waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Wang Yi limefuatia vitisho vya rais wa arekani Donald Trump dhidi ya utawala wa mjini Pyongyang."Majadiliano ndio njia pekee ya kupatikana ufumbuzi" amesema waziri Wang katika mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mwenzake wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault, siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema "mzozo wa Korea ya kaskazini utashughulikiwa."
Yeyote atakaesababisha mzozo katika rasi ya Korea "atabeba jukumu la kihistoria la yatakayotokea" ameshadidia waziri wa mambo ya nchi za nje wa China. Katika kadhia ya mradi wa nuklia wa Korea ya kaskazini,"Mshindi hatokuwa yule mwenye kutoa maneno makali au anaetaka kuonyesha misuli".Vita vikiripuka, matokeo yake yatakuwa kuibuka hali ambayo hakuna atakaejiita mshindi" ameonya waziri Wang. Jamhuri ya umma wa China,inayoangaliwa kama mshirika pekee wa Korea ya kaskazini, inapinga mradi wa nuklea wa utawala wa Kim Jong Un, hata hivyo kila mara imekuwa ikiisihi Marekani ijizuwie.
Kitisho cha jaribio jengine la kinuklea la Korea ya kaskazini
Kwa mujibu wa wadadisi, Korea ya kaskazini inaweza kufanya jaribio jengine la kombora la nuklea kesho itakapoadhimisha miaka 105 ya kuzaliwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo Kim Il Sung.
"Hatua za kijeshi zinazingatiwa" amesema mshauri wa masuala ya kisiasa wa ikulu ya Marekani ambae hakutaja jina lake litajwe na kuongeza anaamini Pyong yang itafanya jaribio jengine ama la kombora alinaloweza kupiga toka bara moja hadi jengine,au la kinuklea.
Jumamosi iliyopita rais wa Marekani ameamuru manuari inayobeba ndege za kivita Carl Vinson iliyosindikizwa na manuari nyengine tatu zilizosheheni mitambo ya kufyetulia makombora na nyambizi kadhaa zielekee katika raas ya Korea.
Mike Pence kuzitembelea nchi za Asia-Pacific
Wakati huo huo makamo wa rais wa Marekani Mike Pence anatarajiwa kuwasilio Korea ya kusini jumapili hii,akianza ziara ya siku kumi katika nchi za Asia Pacific. Mzozo wa Korea ya kaskazini ndio mada kuu atakayoizungumzia atakapokutana na viongozi wa Korea ya Kusini, Japan, Indonesia na Australia.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga