1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza

Oumilkher Hamidou8 Januari 2009
https://p.dw.com/p/GUKD
Vifaru vya Israel katika vita vya GazaPicha: picture-alliance/ dpa



Mada tatu zimehodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo;mzozo wa Mashariki ya kati,Mvutano wa gesi  kati ya Urusi na Ukraine na madhara ya mzozo wa fedha kwa soko la ajira nchini Ujerumani.



Tuanzie lakini Mashariki ya kati ambako gazeti la Münchner Merkur linazungumzia hali ya mambo huko Gaza:Gazeti linaendelea kuandika:


"Hamas wanaweza kudhoofika ikiwa wakaazi wa ukanda wa Gaza watapatiwa  njia nyengine ya matumaini.Kwa namna hiyo walimwengu wasichoke katika juhudi zao za kulifikia lengo hilo.Ushahidi upo tena wa kutosha unaoonyesha matumizi ya nguvu na kulipiza kisasi,hayasaidii kuleta ufumbuzi."


Finacial Times Deutschland linapima uwezekano wa kuwekwa chini silaha japo kwa muda na kuandika:


Hata saa chache za kuweka chini silaha ni ufanisi.Mzizi wa fitina unatokana na Hamas .Ikiwa watawala wa itikadi kali huko Gaza hawataonyesha hamu ya kutaka kuvuta pumzi,basi matumaini  ya kusitisha mapigano japo kwa siku chache,hayatakua mazuri.Kwa mtazamo wa muda mrefu watalazimika kuachia maeneo ya mpakani pamoja na Israel na Misri yawe chini ya usimamizi wa kimataifa.


Kuhusu mzozo wa gesi,gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG linajiuliza:


Wakulaumiwa nani kati ya Urusi na Ukraine kama gesi haipelekwi barani Ulaya?Ingawa kutokana na juhudi za kansela Angela Merkel suala hilo litafafanuliwa hivi sasa na tume huru ya wataalam.Hata hivyo,kwa vyovyote vile matokeo ya ukaguzi huo yatakavyokua,kimoja tangu sasa ni dhahir,Ulaya inabidi isake njia nyengine ya kukidhi mahitaji yake ya gesi,bila ya kutegemea Urusi.Na njia hiyo itapatikana kupitia nishati mbadala."


Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu madhara ya mzozo wa fedha kwa soko la ajira.Gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung linaandika:


Habari mbaya kutoka soko la ajira zinazidi kuchapishwa mwezi hadi mwezi.Na kama ilivyo kawaida katika hali kama hiyo,shinikizo linazidi kuitaka serikali ichukue hatua.Lakini hayo pekee hayatoshi.Hata waajiri na vyama vya wafanyakazi wanabidi wawajibike,wakitaka kuepukana na kitisho cha miaka ya nyuma katika soko la ajira.