1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa Mugabe kupewa heshima katika sehemu tatu tofauti

10 Septemba 2019

Waziri wa habari wa Zimbabwe amesema mwili wa Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe utalazwa katika sehemu tatu tofauti mjini Harare kwa ajili ya kupewa heshima ya kitaifa kabla ya kuzikwa siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/3PKve
Robert Mugabe Simbabwe Afrika ehem. Präsident
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Robert Mugabe kiongozi wa zamani wa Zimbabwe aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 37, alifariki Ijumaa katika hospitali moja nchini Singapore alikokuwa akipata matibabu.

Alikuwa na umri wa miaka 95. Waziri wa Habari wa Zimbabwe Monica Mutsvangwa amefahamisha kwamba mwili wa Mugabe utalazwa katika uwanja wa michezo wa Rufaro mjini Harare siku ya Alhamisi na Ijumaa kwenye uwanja wa michezo wa kitaifa, na siku ya Jumamosi mwili wa kiongozi huyo utalazwa katika Ikulu.

Hata hivyo waziri huyo wa habari alifahamisha tu kwamba marehemu Robert Mugabe atazikwa siku ya Jumapili lakini hakutaja mahala ambapo maziko yatafanyika hali ambayo inaudhihirisha uvumi kwamba kuna hali ya kutokukubaliana kati ya familia ya Mugabe na serikali juu ya mahala atakapozikwa Rais huyo wa zamani wa Zimbabwe.