1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati wa Kenya apatikana akiwa amekufa.

Admin.WagnerD13 Februari 2019

Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini Kenya Caroline Mwatha aliyekuwa akipambana na ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela amepatikana akiwa amekufa siku sita baada ya kutoweka.

https://p.dw.com/p/3DIi0
Kenia Protest vor dem Gerichtsgebäude in Nairobi Prozess gegen zwei Polizisten
Picha: Reuters/T. Mukoya

Taarifa ya Idara ya upelelezi wa jinai nchini Kenya imesema Mwatha alifariki dunia wakati wa jaribio la kutoa mimba aliyokuwa nayo ya miezi mitano, na kwamba watu sita wamekamatwa.

Taarifa hiyo hata hivyo haijaeleza ni kwa nini watu hao walikamatwa, lakini ikasema kikundi hicho ni pamoja na na mmiliki wa kliniki ambayo shughuli hiyo ya kutoa mimba ilifanyika, mtoto wake wa kiume, daktari aliyehusika katika shughuli hiyo na dereva wa taxi.

Msemaji wa polisi Charles Owino amethibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao sita. Aidha polisi wanasema kuwa maiti ya Mwatha ilipelekwa katika hifadhi ya maiti tarehe saba, siku ambayo marehemu anasemekana kutoweka. Kauli inayotiliwa shaka na wanaharakati wengine wa haki za binadamu.

Baba wa marehemu apinga madai ya utoaji mimba

Kenia Nairobi Demonstration Mord an Willie Kimani
Picha: Reuters/T. Mukoya

Hata hivyo Babake pamoja na wanaharakati wengine wa kutetea haki za binadamu wanashikilia kuwa Caroline Mwatha aliuawa kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya mazoea ya polisi kuwauwa vijana bila kujali katika mitaa ya mabanda. Shisia Wasilwa na kina cha taarifa hiyo.

Taarifa ya polisi inasema kuwa mwili wa marehemu uliandikishwa kwa jina tofauti na kwamba wana ushahidi wa jumbe fupi kati yake na daktari aliyehusika kutoa mimba yake.

Na katika kile ambacho huenda kikabadilisha mkondo wa matukio hayo, baba yake marehemu sasa anasema kuwa mwanaye alikuwa akihofia maisha yake katika siku zake za mwisho za uhai wake.

Kuhusu hilo baba wa mawanaharakati huyo amesema "Amepotea kwa sababu ya kufuata ukweli, sio ugonjwa ni ukweli. Alikuwa akitetea vijana, vijana wakishikwa na polisi, Caro ndiye alikuwa akishinda polisi, anashinda kwa polisi akiwatetea vijana waache kuuliwa.”

Alikuwa mwanaharati wa kutumainiwa

Kenia Polizist in Limuru
Picha: picture-alliance/dpa

Vyombo vya habari nchini humo vinasema alitoweka Februari 6 na polisi imesema ilianzisha uchunguzi siku mbili baadaye, na kugundua kuwa alikuwa na mawasiliano kuhusiana na mpango wa kutoa mimba aliyokuwa nayo.

Mwatha alitoweka katika kitongoji cha makazi duni cha Dandora jijini Nairobi ambako aliishi na kuendesha kampeni dhidi ya unyanyasaji wa watu katika vituo vya polisi nchini humo. 

Utoaji mimba ni kosa nchini Kenya, isipokuwa tu mimba hiyo inapokuwa inahatarisha maisha ya mama. Hata hivyo takwimu zinaonyesha kuwa visa laki nne vya utoaji mimba hutekelezwa kila mwaka.

Mwatha alikuwa afisa mkuu katika kituo cha kijamii kinachopigania haki za binadamu cha Dandora. Kabla ya mauti yake, alikuwa akichunguza visa vya kutoweka na mauaji ya kiholela yaliyotekelezwa na polisi dhidi ya wakazi sita wa Dandora Oktoba mwaka uliopita.

Chama cha madaktari kinasema kuwa zahanati inayodaiwa kuwa Mwatha alifika kutafuta huduma haijasajiliwa. Tukio hilo linajiri majuma machache baada ya mfanyakazi wa shirika la habari la Nation kutoweka na kisha maiti yake kupatikana katika hifadhi ya maiti jijini Nairobi.

Matukio hayo, yanachora taswira ya hofu kwa wanaharakati katika taifa linalosifiwa kwa uhuru wa kujieleza.

 

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Dw Nairobi

Mhariri: Iddi Ssessanga