1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel: Mwaka mmoja tangu shambulio la Oktoba 7

7 Oktoba 2024

Israel inaadhimisha siku ya Jumatatu Oktoba 7, mwaka mmoja wa shambulio la wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas, ambalo ni baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Israel.

https://p.dw.com/p/4lUQW
Raia wa Israel wakiomboleza katika siku ya kumbukumbu ya shambulio la Oktoba 7
Raia wa Israel wakiomboleza katika siku ya kumbukumbu ya shambulio la Oktoba 7Picha: Ariel Shalit/AP Photo/picture alliance

Maadhimisho hayo ya mwaka mmoja tangu yalipotokea mashambulizi  ya Hamas yamefanyika Israel na katika miji mingine duniani. Huko Israel, Rais Isaac Herzog ndiye ameongoza sherehe hizo. Ilipotimia saa kumi na mbili na dakika 29 asubuhi, kulishuhudiwa dakika mmoja ya ukimya ili kuwakumbuka wote waliouawa siku hiyo.

Sherehe rasmi zilifanyika kusini mwa Israel katika vitongoji vya  Kibbutz Reim , kulikokuwa na tamasha la muziki la Nova ambapo takriban watu 370 waliuawa  eneo hilo. Rais Herzog amesema:

"Hili ni kovu dhidi ya ubinadamu. Hili ni kovu kwenye uso wa ulimwengu. Na dunia inabidi itambue na kufahamu kwamba ili kuibadilisha historia, kuleta amani na mustakbali mwema wa eneo la mashariki ya kati, ni lazima kuiunga mkono Israel katika vita vyake dhidi ya maadui zake. Tunapigana vita vya kuuweka ulimwengu huru."

Rais wa Israel Isaac Herzog
Rais wa Israel Isaac HerzogPicha: Artur Widak/AA/picture alliance

Shambulio la Oktoba 7, lililoua watu 1,205 na kuwachukua mateka mamia ya wengine kwa mujibu wa takwimu rasmi za Israel, lilisababisha kiwewe ambacho bado kinawaandama waIsrael wengi. Mamlaka za Israel zimeimarisha usalama kutokana na hofu ya kutokea mashambulizi mengine kama hayo, hasa siku hii ya kumbukumbu.

Soma pia: Israel yashambulia ngome za Hezbollah mjini Beirut

Mjini Tel Aviv, familia za mateka walikusanyika mbele ya makazi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wakitoa wito wa kufanyika juhudi za ziada ili kurejeshwa nyumbani wapendwa wao, ambao ni mateka waliosalia mikoni mwa Hamas. Netanyahu amesema katika mwaka mmoja uliopita, jeshi la nchi yake limebadili hali halisi katika eneo hilo.

Kumbukumbu zafanyika sehemu mbalimbali duniani

Wajerumani wakiandamana kudhihirisha uungwaji mkono kwa Israel
Wajerumani wakiandamana kudhihirisha uungwaji mkono kwa IsraelPicha: Ralf Hirschberger/AFP/Getty Images

Kumeshuhudiwa matukio mbalimbali kote duniani ili kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Hamas lakini baadhi yamekuwa pia yakidhihirisha uungaji mkono kwa watu wa Palestina ambao wanakabiliwa na maafa makubwa baada ya mwaka mmoja wa vita huko Gaza ambavyo kwa mujibu wa wizara ya afya watu 41,909 wameuawa. Mpalestina Nabeel Abu Al Fahim amesema:

"Oktoba 7 ni siku ya kihistoria ambayo Waisraeli na Wapalestina hawataisahau. Hapa tuna njaa na janga kutokana na uharibifu wa miundombinu, tunakabiliwa na matatizo ya maji, dawa, matibabu, makazi na maji ya kunywa."

Soma pia: Umetimia mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7

Maadhimisho hayo yanakuja huku Israel ikiwa bado inapambana vikali na Hamas huko Gaza, huku ikiwa imeanzisha vita vipya nchini Lebanon dhidi ya kundi la Hezbollah. Israel inajiandaa pia kulipiza kisasi dhidi ya Iran kufuatia shambulio la wiki iliyopita la Tehran na hivyo kuzidisha hofu ya kutokea vita vipana zaidi vya kikanda.

(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)