1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mursi akata mahusiano na Syria

16 Juni 2013

Rais wa Misri Mohammed Mursi amesema kuwa amekata uhusiano wote wa kidiplomasia na utawala wa mjini Damascus, na kutoa wito wa kuundwa kwa eneo la marufuku ya kuruka ndege nchini Syria.

https://p.dw.com/p/18qg9
Rais wa Misri, Mohammed Mursi
Rais wa Misri, Mohammed MursiPicha: Imago

Akihutubia mkutano uliyoitishwa na viongozi wa dini wa madehehebu ya Sunni mjini Cairo, rais Mursi aliwaonya pia washirika wa rais Bashar al-Assad, kundi la Kishia la Lebanon linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah, na kulitaka kuondoka mara moja kutoka nchini Syria. "Hezbollah laazima waondoke Syria, haya ni maneno mazito," alisema Mursi, ambae nchi yake ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa kisunni wiki hii, ambao walitoa wito wa vita vya jihadi dhidi ya Damascus.

Wafuasi wa rais Mohammed Mursi kutoka chama cha Udugu wa Kiislamu
Wafuasi wa rais Mohammed Mursi kutoka chama cha Udugu wa KiislamuPicha: Mahmud Hams/AFP/GettyImages

Tofauti za wazi kati ya wasunni na washia

"Hakuna nafasi ya Hezbollah ndani ya Syria," alisema Mursi. Mkutano huo ulionyesha mgawanyiko mkubwa wa kidini unaoikumba kanda hiyo. Kiongozi mmoja aliezungumza kabla ya rais Mursi aliwataja Washia kama wazushi, makafiri, madhalimu na washirikina. Mkutano huo pia ulitumika kuonyesha mshikamano na Mursi, wakati ambapo wapinzani wake wakiandaa maandamano ya kudai kuitishwa uchaguzi wa mapema wa rais.

Mursi alipeperusha bendera za Misri na Syria wakati akiingia ukumbi uliyokuwa na wafuasi wake wapatao 20,000. Umati ulikuwa ukiimba: "Kutoka kwa wanamapinduzi huru wa Misri: Tutagonga mhuri juu yako Bashar!" Mursi, ambae ni mwanasiasa wa chama cha Udugu wa Kiislamu, alijitenga na kutoa matamshi ya moja kwa moja kuhusu Washia na Iran, lakini katika sehemu ya dokezo kwa Iran, aliyatuhumu mataifa katika kanda hiyo na ya mbali kwa kuendesha "kampeni ya ukatili na mauaji ya kikabila" nchini Syria.

"Tumeamua leo kukata kabisaa mahusiano na Syria na utawala wa sasa wa Syria," alisema Mursi. Aliyataka pia mataifa makubwa duniani kutosita kuweka kanda ya marufuku ya kuruka ndege katika anga ya Syria. Wanadiplomasia wa magharibi walisema siku ya Ijumaa kuwa Marekani ilikuwa inafikiria kuweka kanda hiyo katika baadhi ya maeneo ya Syria, lakini ikulu ya White House ilisema baadae kuwa Marekani haikuwa na maslahi ya kitaifa katika kutekeleza jambo hilo.

Raia wa Syria waliokimbia mapigano na kuingia nchini Uturuki katika mkoa wa Hatay.pixel Schlagworte fliehen , Ventilator , Flüchtlinge , Habseligkeiten , Grenze , neu , Syrien , Politik , Krisen , Gesellschaft pixel Überschrift Syrische Flüchtlinge ... Personen Kontinent - Land Türkei Provinz - Ort Hatay Aufnahmedatum 20120813 pixel Rechtliche Daten Bildrechte Verwendung nur in Deutschland Besondere Hinweise - Rechtevermerk picture alliance / abaca Notiz zur Verwendung picture alliance / abaca pixel
Raia wa Syria waliokimbia mapigano na kuingia nchini Uturuki katika mkoa wa Hatay.Picha: picture alliance/abaca

Urusi, ambayo ni mshirika wa Assad na mpizani mkubwa dhidi ya kuingilia kijeshi nchini Syria, ilisema kuweka marufuku ya kuruka ndege kwa kutumia ndege za kivita aina ya F-16 na makombora ya Patriot vilivyoko nchini Jordan itakuwa kinyume na sheria. Mursi alisema alikuwa anaandaa mkutano wa dharura wa mataifa ya Kiarabu na mengine ya Kiislamu kujadili hali nchini Syria, ambako Marekani imeamua kuchukua hatua zaidi kwa kuwapatia silaha waasi.

Jeshi la Misri linalofadhiliwa na kupewa mafunzo na Marekani ni miongoni mwa majeshi yenye nguvu zaidi katika mashariki ya kati. Hata hivyo hakujatolewa pendekezo lolote kwamba Misri, ambayo inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kwa sasa, ijiingize katika mapigano ndani ya Syria.

Aonya dhidi ya vurugu

Mursi alisema: "Watu wa Misri wanaunga mkono mapambano ya watu wa Syria kwa hali na mali, na Misri, taifa lake, uongozi....na jeshi, hawatawaacha watu wa Syria hadi watakapopata haki zao na heshima yao." Udugu wa Kiislamu umeungana na mashirika mengine ya madhehebu ya kisunni kutoa wito wa vita vya dini dhidi ya Assad na washirika wake wa Kishia.

Misri haijashiriki kikamilifu katika kuwapatia silaha waasi wa Syria, lakini msaidizi mmoja wa Mursi alisema wiki hii kuwa serikali mjini Cairo haitawazuia raia wa nchi hiyo wanaotaka kupigana nchini Syria. Hii ilikuwa hotuba ya pili ya uchokozi kutolewa na Mursi katika kipindi cha wiki moja. Siku ya Jumatatu, alisema anaacha njia zote wazi katika kushughulikia mgogoro na Ethiopia kuhusiana na bwawa kubwa la umeme ambalo Ethiopia inajenga katika mto Nile, ingawa alisema Cairo haitaki vita na kusisitiza kuwa atatumia njia za kidiplomasia.

Raia wa Misri wakiandamana kupinga kuingilia kwa Hezbollah katika vita vya Syria.
Raia wa Misri wakiandamana kupinga kuingilia kwa Hezbollah katika vita vya Syria.Picha: picture-alliance/AP

Wapinzani wa Mursi - waliberali na wanasiasa wa mrengo wa kushoto wanaanda maandamano makubwa Juni 30, tarehe ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu Mursi alipoingia ofisini, na kuchochea hofu ya kuwepo vurugu zaidi. Mursi aliwambia wafuasi wake wakati wa mkutano kwamba wasikubali kuingizwa katika malumbano, na kwamba hatavumilia vurugu zozote.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre.
Mhariri: Sudi Mnette