1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe kuitisha uchaguzi mpya Zimbabwe miaka miwili ijayo

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP26 Februari 2009

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema kuwa huenda akaitisha uchaguzi mkuu mpya katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

https://p.dw.com/p/H20i
Rais Robert MugabePicha: picture-alliance/ dpa



Akizungumza katika mahojiano na gazeti la serikali yake la The Herald, Rais Mugabe pia amekataa kutengua uamuzi wa kuwateua tena gavana wa benki kuu pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu.


Rais Mugabe mwenye umri miaka 85 amesema kuwa serikali mpya ya umoja iliyoundwa wiki mbili zilizopita kwa kugawana madaraka na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ni suluhisho la muda, kwani suluhisho kamili ni mpaka vyama vyao vitakapokubaliana juu katiba na uchaguzi mpya.

Amesema kuwa vyama vinavyounda serikali hiyo vimekubaliana kuandaa rasimu ya katiba mpya ambayo itapigiwa kura ya maoni katika kipindi cha miaka miwili ijayo.


Amesema kuwa mara baada ya kura hiyo ya maoni juu ya rasimu ya katiba mpya ndipo utaitishwa uchaguzi mpya.


Zimbabwe ilianza kutumbukia katika mzozo wa kisiasa na kiuchumi miaka minane iliyopita wakati Rais Mugabe aliposhindwa katika kura ya maoni juu ya katiba mpya ambayo ilikuwa inataka kutoa nafasi kwa rais huyo aendelee kukaa madarakani.Mugabe ameiongoza Zimbabwe toka ilipopata uhuru wake mwaka 1980.


Tsvangirai ambaye ni hasimu wa muda mrefu wa Mugabe alikubaliana kuingia katika serikali ya umoja kufuatia mbinyo mkubwa wa jumuiya ya kimataifa kwa Rais Mugabe kumtaka akubaliane na upande wa upinzani kuunda serikali hiyo.


Serikali hiyo mpya inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza mfumko mkubwa kabisa wa bei nchini humo, na kuufufua uchumi ambao umepelekea asilimia 94 ya watu wote kutokuwa na ajira.


Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai tayari amepinga hatua ya Rais Mugabe kumteua tena Gideon Gono kuwa Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.


Gono amekuwa gavana wa benki kuu ya Zimbabwe katika kipindi ambacho kimeshuhudia sarafu ya nchi hiyo dola ikishuka thamani kwa kiwango kikubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa.


Mugabe pia amewatua maafisa wengine wa juu katika idara mbalimbali bila ya kumshirikisha Waziri Mkuu, hatua ambayo Morgan Tsvangirai amesema ni ukiukaji wa mkataba wao wa kugawana madaraka.


Katika mahojiano hayo Rais Mugabe pia amekanusha uvumi ya kwamba nchi hiyo huenda ikaamua kutumia sarafu ya Afrika Kusini Rand, badala ya sarafu ya nchi hiyo dola ambayo wafanyabishara na wa chuuzi wengi wanakataa kuipokea.


Aidha amesema kuwa anapinga fikra za kulipa mishahara ya watumishi wa umma kwa kutumia fedha za kigeni.


Ikumbukwe ya kwamba mara baada ya kuingia madarakani Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai aliamua watumishi wote wa umma kulipwa marupurupu kwa fedha za kigeni hatua ambayo ilipelekea waalimu waliyokuwa katika mgomo kwa takriban mwaka mmoja kukubali kurejea kazini.


Tsvangirai ametoa ombi kwa jumuiya ya kimataifa kuipatia kiasi cha dola billioni tano ili kuusaidia uchumi wa Zimbabwe na kuzikarabati sekta za afya na elimu vilivyoathiriwa na mzozo wa muda mrefu wa kisiasa nchini humo.


Nchi wafadhili za magharibi ambazo zinafadhili miradi mingi ya kibinaadamu nchini Zimbabwe zimeonesha nia ya kutoa misaada yao lakini mpaka pale Rais Mugabe atakapo thibitisha kivitendo kwamba yuko tayari kugawana madaraka na upinzani.



Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo siku ya Jumatano alitoa wito kwa Rais Mugabe kusikilia kilio cha jumuiya ya kimataifa na kumtaka kuwaachia wafungwa wote wa kisiasa ikiwa ni alama ya kuthibitisha kwamba yuko tayari kwa serikali ya umoja.