1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mswada wa mwisho wa mabadiliko ya tabia nchi kuwasilishwa

Sekione Kitojo
13 Desemba 2018

Mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoonekana kuwa majadiliano muhimu zaidi ya Umoja wa Mataifa tangu makubaliano  ya  Paris yako katika wiki ya mwisho mjini Katowice, nchini  Poland.

https://p.dw.com/p/3A3ki
Polen | COP 24 United Nations Climate Conference
Picha: picture-alliance/dpa/ZUMAPRESS

Rais  wa  mkutano  huo  kutoka  Poland anatarajiwa kuwasilisha  mswada  wa waraka  wa  mwisho ambao utajumuisha  sheria maalum za  utekelezaji  wa  makubaliano  ya Paris, makubaliano  juu  ya kugharamia  mabadiliko  ya  tabia  nchi na  mkataba  mwingine  wa  kuongeza  juhudi  za  kuzuwia  utoaji  wa gesi  zinazochafua  mazingira.

UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Pavillion Indonesien
Wajumbe wa majadiliano ya COP 24 wakiangalia vitu mbali mbali katika mabanda ya maoneshoPicha: DW/N. Langjahr

Mswada  huo  utawasilishwa  kwa  wajumbe   na  mawaziri watafanyakazi  kuweza  kupata  waraka  utakaoweza  kukubalika ifikapo  mwisho  wa  mkutano  huo kesho  Ijumaa. "Maelezo yanapaswa  kuchujwa  na  tunapaswa  kuangalia  wapi  tunakutana kwa  vipande tofauti  vya  waraka  huu, lakini  hatujafika  huko  hadi sasa,"  amesema  hivyo Jennifer Morgan, mkurugenzi  mtendaji  wa shirika  la  Greenpeace  International.

"kila  nchi  hapa  inahitaji  kuchukua  hatua moja  nyuma na kukumbuka  kwa  nini  tuko  hapa.  Uhai  wetu uko  hatarini.

Wajumbe kufikia  makubaliano Katowice

Bado  haijafahamika  ni  vipi  wajumbe  watakamilisha  makubaliano ya  utekelezaji  wa  makubaliano  ya  Paris, ambayo  yanalenga kubakisha  ongezeko  la  ujoto  kuwa  chini  ya  nyuzi  joto mbili  juu ya  nyakati  kabla  ya  enzi  za  viwanda, na  iwapo  waraka  huo utatilia  maanani ripoti  ya  hivi  karibuni  ya  jopo la Umoja  wa Mataifa  linaloundwa  na  muungano  wa  serikali  mbali  mbali kuhusu  mabadiliko  ya  tabia  nchi IPCC.

UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Pavillion Indonesien
Wajumbe katika mkutano wa UN wa mazingira mjini KatowicePicha: DW/N. Langjahr

Mataifa  ambayo  yanakabiliwa  na  athari  kubwa  za  mabadiliko  ya tabia  nchi  yametaka  mkutano  huo  kutoa  ujumbe  mzito  kwamba dhamira  ya  dhati  ya  kupunguza  utoaji  wa  gesi  zinazoharibu mazingira  duniani  ni  lazima kuimarishwa  ifikapo  mwaka  2020.

Visiwa  vya  Maldives vitafanya  kila  linalowezekana  katika  uwezo wake  kuzuwia  maji  kukimez  kisiwa  hicho, mkuu  wa  ujumbe  wa nchi  hiyo  katika  mkutano  huo  amesema  leo  katika  hali  ya kutoa  wito  kwa  mataifa  kuondoa  tofauti  zao  kuhusiana  na  jinsi gani  ya  kupambana  na  ongezeko  la  ujoto  duniani.

Euroclima Konferenz in COP24
Majadiliano yakiendelea katika mkutano wa mazingira wa UN mjini KatowicePicha: DW/J. Alonso

"Hatuko tayari  kufa. Hatutakuwa  wahanga  wa  kwanza  wa  mzozo wa  mazingira. Badala  yake , tutafanya  kila  kitu  katika  uwezo wetu  kuweka  vichwa  vyetu  juu  ya  maji," Mohamed Nasheed aliwaambia  wajumbe  katika  mazungumzo  hayo  ya  Katowice , nchini  Poland.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Josephat Charo