Mshtuko wa Brexit bado waipiga Ulaya
4 Julai 2016Katika kura ya maoni iliyofanyika Juni 23 asilimia 52 ya Waingereza waliamua kuunga mkono kujitowa katika Umoja wa Ulaya wakati asilimia 48 ya wananchi wa taifa hilo walipiga kura ya kuupinga uamuzi huo-Lakini matokeo hayo yalisababisha mtikisiko mkubwa wa masoko ya fedha duniani na kuzusha wasiwasi kuhusu hatma ya Umoja wa Ulaya.
Kufuatia wimbi hilo la wasiwasi uliouzonga Umoja huo wa Ulaya kwa hivi sasa zinasikika sauti kutoka kwa viongozi mbali mbali pamoja na wanasiasa wa ngazi za juu katika Umoja huo wakizungumzia nini kinachotakiwa kufanyika kuukoa Umoja huo.Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble akihojiwa hapo jana na kituo kimoja cha hapa Ujerumani alisema uamuzi uliochukuliwa na Waingereza ni ujumbe wa kuionya Ulaya izinduke kutoka kwenye usingizi mzito kuhusu matatizo yanayoshuhudiwa na wananchi wake.
Schaaeuble ametilia mkazo kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa sasa kulishughulikia haswa suala la wakimbizi ili urudishe imani kwa wananchi wake .
Kwa upande mwingine waziri wa Uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel ametowa mwito kwa kupunguzwa kwa makamishna katika Umoja wa Ulaya pamoja na kudurusiwa upya jinsi mpangilio wa bajeti ya Umoja huo ulivyo.Ndani ya Uingereza kwenyewe Scotland inaonekana kushikilia dhamira yake ya kutaka kuitisha tena kura kwa mara ya pili juu ya kujitenga na Uingereza.
Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon amesema nchi yake iliyopiga kura kuunga mkono kubakia katika Umoja wa Ulaya katika kura ya Brexit haipaswi kunyimwa nafasi nyingine ya kufanya uamuzi juu ya kubakia au kutobakia ndani ya Uingereza.
Hata kiongozi wa chama cha waziri mkuu David Cameroon cha Consevartive nchini Scotland Ruth Davidson naye amezungumzia msimamo wake na kusema kwamba serikali ya Uingereza mjini London haipaswi kuikatalia Scotland kuitisha kura ya maoni juu ya uhuru wake.Kadhalika katika kinyang'anyiro cha kuwania inayoachwa na waziri mkuu David Cameroon waziri wa mambo ya nje Phillip Hammond amejitokeza kumuunga mkono waziri wa ndani Theresa May kutwaa wadhifa huo akisema anauwezo wa kuifanya Uingereza kufikia makubaliano bora na Umoja wa Ulaya baada ya Talaka ya Brexit.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga