1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa London alizaliwa kama Adrian Russel Ajao

24 Machi 2017

Afisa wa juu wa kupambana na ugaidi mjini London, amesema Khalid Masood aliyeshambulia katika Bunge la Uingereza na kuwaua watu wanne na kuwajeruhi wengine 50 alizaliwa akiwa anaitwa Adrian Russel Ajao.

https://p.dw.com/p/2ZsPY
Großbritannien Terroranschlag in London | Mark Rowley, Scotland Yard
Picha: picture-alliance/dpa/L. Hurley

Afisa wa juu wa kupambana na ugaidi mjini London, amesema Khalid Masood aliyeshambulia katika Bunge la Uingereza na kuwaua watu wanne na kuwajeruhi wengine 50 alizaliwa akiwa anaitwa Adrian Russel Ajao.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, mkuu wa idara ya kupambana na ugaidi mjini London, Mark Rowley amesema mshambuliaji huyo alizaliwa kusini mashariki mwa jiji la London na hivi karibuni amekuwa akiishi katikati ya mji wa Birmingham.

Polisi imesema Khalid Masood ni mzaliwa wa Uingereza aliyebadili dini na kuwa Muislamu, pia alitumia majina kadhaa ya utani na wanajaribu kuona iwapo kuna watu wengine waliomuelekeza kufanya shambulizi hilo. Rowley amesema uchunguzi wao umejikita zaidi katika kutafuta lengo la shambulizi hilo pamoja na kuwabaini washirika wake.

Großbritannien London Trafalgar Square Gedenken
Wananchi wa Uingereza wakiwaomboleza waliouawaPicha: Reuters/S. Wermuth

''Wakati bado hakuna ushahidi wa vitisho zaidi, utaelewa kwamba nia yetu ni kutafuta iwapo alifanya shambulizi hili peke yake, aliongozwa pengine na propaganda za kigaidi, au kama kuna watu wengine walimshawishi, kumuunga mkono au kumuelekeza,'' alisema Rowley.

Watu wawili zaidi wakamatwa

Wakati hayo yakijiri, Rowley amesema polisi wamewakamata watu wawili zaidi usiku wa kuamkia leo, ambapo mmoja amekamatwa West Midlands na mwingine kusini magharibi mwa Uingereza. Amesema kwa sasa polisi inawashikilia jumla ya watu tisa wakihusishwa na shambulizi hilo lililotokea siku ya Jumatano. Hata hivyo, amesema mwanamke mmoja waliyekuwa wanamshikilia, ameachiwa kwa dhamana.

Mshambuliaji huyo aliliendesha kwa kasi gari lake katika umati wa watu kwenye Daraja la Westminster mchana wa Jumatano na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine 50, kabla ya kumuua kwa kumchoma kisu afisa polisi katika eneo la bunge. Hata hivyo mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Majeruhi wawili wako katika hali mbaya, huku mmoja majeraha aliyonayo yakiwa yanatishia uhai wake.

Belgien Polizeieinsatz - Terrorverdacht in Antwerpen
Polisi wa Antwerp, Ubelgiji wakifanya doriaPicha: picture-alliance/dpa/BELGA/V. Lefour

Wakati huo huo maafisa wa usalama nchini Ubelgiji jana wamemkamata mtu aliyeliendesha gari lake kwa kasi katika eneo la maduka mjini Antwerp. Polisi wamepata bunduki na silaha nyingine kama vile visu na mapanga ndani ya gari la mtuhumiwa huyo aliyetambuliwa na waendesha mashtaka kama Mohamed R., mwenye umri wa miaka 39. Mtuhumiwa huyo aliyejaribu kukimbia, alikamatwa katika mji wa kaskazini.

Ofisi ya mwendesha mashtaka imesema mtuhumiwa huyo ni raia wa Ufaransa, ingawa duru za polisi nchini Ufaransa zimeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba alikuwa ana asili ya Tunisia anayeishi kihalali kwenye mji wa Ufaransa wa Lens, ulioko karibu na mpaka wa Ubelgiji. Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel amesema idara ya usalama imefanya kazi nzuri sana na serikali inalifatilia kwa karibu na umakini mkubwa tukio hilo la kushangaza.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga