Msaada wa Ugiriki kuchelewa
21 Novemba 2012Mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa nchi 17 za umoja wa Ulaya zinazotumia Euro Jean-Claude Juncker amesema mazungumzo zaidi yataendelea jumatatu. Amesema bado ana uhakika kwamba misaada itaanza kutolewa hivi , na kwamba kikao hicho kimeweza kupiga hatua ya kubainisha fungu litakalosaidia serikali ya Ugiriki katika suala la madeni.
Jean-Claude Juncker amewaambia waandishi wa habari mjini Brussels kuwa'' tunakaribia kupata matokeo pasipo kuwapo na kikwazo'' akaongeza kuwa ''Nimekatishwa tamaa kidogo lakini lazima nikiri kuwa masuala ya kiufundi yana ugumu wake''. alisema kiongozi huyo.
Wakati ameulizwa ni lini Ugiriki itapata sehemu ya mkopo, mwenyekiti huyo alisema hajui ni lini hilo litatokea. Lakini akaongeza kuwa Ugiriki itapata mkopo na hiloanalo uhakika litatokea.
Jinsi gani mgogoro utatatuliwa?
Suala kubwa linalotakiwa kutatuliwa ni jinsi gani ya kuziba pengo la euro bilioni 32.6 sawa na dola 41.7 katika mfuko wa uokozi wa Ugiriki ambao ulitengenezwa baada ya mawaziri wiki iliyopita kukuabaliana kuipatia nchi hiyo miaka miwili zaidi kurejesha hali yake ya kifedha katika mstari.
Waziri wa fedha wa Austria Maria Fekter amesisitiza kabla ya mkutano huo kwamba alitaka kuona''hakuna fedha mpya kwa sababu ni vigumu kuwaelezea walipa kodi''. Njia nyingine ni kukata kiwango cha riba ya Ugiriki ama kuongeza muda wa mikopo yake.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble alisema ''Tunao mfulilizo wa njia tofauti za namna ya kuziba hilo pengo, Tumejadili kwa kina , hata hivyo kwa kuwa maswali ni magumu tumeshindwa kufikia suluhisho''. alisema waziri huyo.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la fedha duniani IMF, Christine Lagarde amesema wanakaribia kuziba pengo hilo lakini bado hawajafikia.
IMF na Umoja wa Ulaya pia zimeshindwa kukubaliana endapo Ugiriki inatakiwa kwenda mpaka mwaka 2020 au mwaka 2022 katika kupunguza madeni yake kwa asilimia 120 ya pato la taifa.
Kwa ujumla mawaziri hao wanajaribu kuamua namna bora ya kushughulikia madeni ya Ugiriki ambayo kwa sasa yanatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 190 ya pato la taifa kwa mwaka ujao.
Ugiriki kwa sasa ilikuwa na matumaini ya kupokea euro bilioni 31.5 kama sehemu ya mkopo na fedha hizo zilipaswa kutolewa mwezi Juni lakini zikachelewa wakati serikali ya Ugiriki ilipokuwa ikajaribu kufikia masharti na mpango wa mageuzi unaotakiwa na wakopeshaji.
Mwandishi:Sylvia Mwehozi/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman