1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wawaua kiasi ya watu 27 katika Kilabu Romania

31 Oktoba 2015

Mripuko uliotokea jana Ijumaa usiku katika kilabu kimoja mjini Bucharest nchini Romania, umewaua kiasi ya watu 27 na kuwajeruhi kiasi ya watu wengine 180.

https://p.dw.com/p/1GxVk
Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya ndani wa Romania Gabriel Oprea amesema mripuko huo ulitokea katika kilabu ya Colectiv iliyokuwa na kati ya wateja 300 na 400 wengi wao vijana.

Mripuko huo unaaminika ulitokea wakati wanamuziki wa bendi ijulikanayo Goodbye to Gravity, walipokuwa wakiimba na kulikuwa na maonyesho ya kutumia baruti.

Kituo cha televisheni cha Antena 3 kimeripoti kulikuwa na mlango mmoja tu wa kutokea katika kilabu hiyo. Rais Klaus Iohannis amesema ameshtushwa na kuhisi machungu kutokana na mkasa huo na ametuma salamu za rambi rambi.

Rais ahuzunishwa na mkasa huo

Rais Iohannis amesema anatafakari kutangaza siku ya kitaifa ya maombolezi. Wizara ya afya imetoa wito watu wajitokeze kutoa damu kuwasaidia majeruhi. Waziri mkuu wa Romania Victor Ponta ambaye yuko ziarani Mexico amesema anakatisha ziara yake na kurejea Bucharest baada ya mkasa huo.

Rais wa Romania Klaus Iohannis
Rais wa Romania Klaus IohannisPicha: Reuters/R. Sigheti

Duru kutoka hospitali zinaarifu kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kwasababu kiasi ya majeruhi 25 wako katika hali mahututi. Afisa wa Romania Raed Arafat amesema mkasa huo ni miongoni mwa mibaya zaidi kuwahi kuukumba mji huo mkuu wa Romania.

Mkuu wa hospitali kuu ya Bucharest Monica Pop amesema wamepokea vijana wa kati ya umri wa miaka 14 hadi 16 walio na majeraha ya moto. Walioshuhudia mkasa huo wamenukuliwa na vyombo vya habari kuwa kulizuka tafrani baada ya baruti na fataki zilizowashwa katika tamsha hilo la muziki kuunguza nguzo moja ya ukumbi huo na kusambaa hadi darini.

Wengi wa waathiriwa ni vijana wadogo

Umati uliingiwa na hofu wakati moshi mkubwa ulipoghubika ukumbi huo na kusababisha mkanyagano kila mmoja akijaribu kukimbilia usalama wake kupitia mlango mmoja wa kilabu hiyo.

Kulingana na maafisa wa afya wengi wa majeruhi wana majeraha ya miguu,kuungua na madhara mengine baada kuvuta moshi. Polisi imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho. Waziri wa mambo ya ndani Gabriel Oprea amesema mkutano wa dharura umeitishwa hii leo kuujadili mkasa huo.

Kufuatia taarifa za mkasa huo,watu kadhaa wamewasili katika kilabu hiyo kuwatafuta jamaa zao huku kukiwa na hofu kuwa wengi wa waliokuwa wanahudhuria tamasha hilo la muziki hawakuwa na vitambulisho na hivyo ni vigumu kuwatambua.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Isaac Gamba