Mpango wa kuwahudumia wakimbizi Uganda wakumbwa na ufisadi
30 Novemba 2018Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wake uliopongwezwa sana juu ya wakimbizi nchini Uganda, umegundua ufisadi wa mamilioni ya dola na kutowajibika.
Ripoti ya idara ya ukaguzi wa huduma za ndani ya Umoja huo, umeonesha malipo yalioongezwa hesabu, rushwa na udanganyifu, huku sheria zikikiukwa na kusababisha hasara kwa Shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa.
Uganda inawahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni moja ambao wameikimbia Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kutoka nchi nyengine.
Nchi hiyo imekuwa ikipongezwa kwa kuwa sera yake ya kuwafungulia milingo wakimbizi na kuwaruhusu kuwa na uhuru wa kutembea nchini humo, kuweza kupata huduma za afya, pamoja na ardhi ndogo kwa ajili kilimo na makazi.
Shirika hilo la Ukaguzi la Umoja wa Mataifa limechunguza shughuli za Shirika linalowahudumiwa wakimbizi la Umoja wa Mataifa -UNHCR nchini Uganda kwa miezi 18 kuanzia Julai 2016.