Mpango wa dolla bilioni 700 unaolengwa kuyanusuru masoko ya Fedha waendelea kujadiliwa
28 Septemba 2008Wabunge wa Marekani wamefikia makubaliano kiasi fulani kuhusu mpango wa dolla billioni 700 unaotazamiwa kunusuru masoko ya fedha ya taifa hilo.
Spika wa bunge la wawakilishi Nancy Pelosi amewaambia waandishi wa habari kwamba mpango huo lakini unabidi kujadiliwa zaidi kabla ya kufikiwa makubaliano rasmi.
Kwa upande mwingine kiongozi wa baraza la Senate ambaye ni mbunge wa chama cha Demokrat Harry Reid amesema watalikamilisha suala hili na wataendelea kulijadili kwa kadri itakavyohitajika kulikamilisha na kwamba watashirikiana na rais Bush kurekebisha mpango wake huo ili kuufanya uwe bora zaidi kwa walipa kodi na wenye kumiliki nyumba na wanataka kuhakikisha kwamba mpango huu unapitiwa.
Wabunge wamekuwa wakiujadili mpango huo ambao unakosolewa kwa kukosa uwajibikaji tangu jana na wanatarajia kufikia makubaliano kamili jumatatu wakati wa kufunguliwa kwa masoko ya hisa.
Mpango huo ambao umependekezwa na utawala wa rais George Bush unataka kutumia fedha za walipa kodi wa Marekani kununua mikopo mibaya ya mabenki ambayo ndio chanzo za mzozo huo wa masoko ya fedha.