1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Monrovia. George Weah anaongoza.

16 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CERT

Mwanasoka tajiri George Weah amekuwa anaongoza mbio za kuwania kiti cha urais nchini Liberia hadi jana Jumamosi, huku kura kutoka asilimia 80 ya majimbo ya uchaguzi nchini humo zikiwa zimehesabiwa, lakini duru ya pili ya uchaguzi bado inaonekana suala ambalo haliepukiki.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa AC Milan , Weah amepata asilimia 29.8 ya kura kutokana na matokeo yaliyopatikana kutoka katika vituo 2,457 vya uchaguzi kati ya vituo 3,070.

Ellen Johnson – Sirleaf, mwanauchumi wa zamani katika benki kuu ya dunia ambaye anaweza kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kuwa rais iwapo atashinda , yuko katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 19.7 ya kura.

Mgombea anatakiwa kupata asilimia 50 ili kuweza kupata ushindi wa moja kwa moja katika duru ya mwanzo, la sivyo uchaguzi wa pili utafanyika kati ya wawili ambao wamepata asilimia za juu kuliko wengine.