Klingbeil: Jeshi la Iran liwekwe kwenye orodha ya magaidi
12 Machi 2023Kiongozi mwenza wa chama tawala cha Social Democrats cha Ujerumani, Lars Klingbeil, ameishtumu Iran kwa hatua yake ya kumhukumu mwanafunzi kijana na kutoa wito kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, IRGC, kuwekwa kwenye orodha ya Umoja wa Ulaya kuwa ni shirika la kigaidi.
Mwanasiasa huyo wa Ujerumani amesema ameshtushwa na hukumu iliyotolewa dhidi ya Samaneh Asghari, mwanafunzi aliyekuwa akisomea shahada ya uhandisi na ambaye alimpa ufadhili wa kisiasa mnamo mwezi Januari.
Klingbeil ameliambia shirika la habari la Ujerumani la Funke katika maoni yaliyochapishwa leo Jumapili kuwa, IRGC inapaswa kuwekwa kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.
Ameeleza kuwa, utawala wa Iran umetoa hukumu ya miaka 18 na miezi mitatu jela dhidi ya Samaneh Asghari kutokana na shutuma zisizokuwa na msingi wowote.
Jeshi hilo lilianzishwa mnamo mwaka 1979 ili kuzuia kufanyika kwa mapinduzi na pia kuutetea mfumo mpya wa Kiislamu.