Mkutano wa kilele wa umoja wa Afrika
31 Januari 2011Mada kuu zotakazojadiliwa leo Sudan baada ya kura ya maoni, na mustakabali wa Somalia baada ya kumalizika muda uliowekwa kwa serikali ya mpito hapo mwezi Agosti mwaka huu.
Mkutano huo wa Umoja wa Afrika unaongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika akiwemo Rais wa Sudan, Omar al Bashir, Rais wa Sudan ya kusini, Salva Kiir, Waziri mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping.
Akizungumzia Somalia, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye pia atakutana na Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, Sharif Sheikh Ahmed, amesema licha ya mizozo mingi inayolikabili bara la Afrika kwa sasa, Somalia bado haijasahaulika.
Amesema Wasomalia wameteseka muda mrefu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyosababishwa pia na kutokuwepo kwa umadhubuti wa kisiasa kwa takriban miaka 20 sasa nchini humo.
Akizungumzia suala la Sudan, Ban Ki Moon amesema cha muhimu sasa ni kwa pande zote kushughulikia haraka masuala yanayojitokeza baada ya kura ya maoni ya Sudan ya kusini, ambayo ni suala la mpaka kati ya kusini na kaskazini, uraia masuala ya usalama na ushirikiano wa rasilimali zilizopo na pia suala la wilaya iliyoko mpakani ya Abyei.
Maafisa tayari wameshatangaza kwamba zoezi la kura ya maoni Sudan ya kusini lilienda vizuri kwa karibu asilimia 99 ya Wasudan kusini waliopiga kura walitaka kujitenga. Hiyo ni kwa mujibu ya matokeo yaliyotangazwa jana.
Mkutano huo pia utaujadili pia mkoa wa Darfur, uliko Sudan magharibi, katika harakati za kurejesha amani.
Mbali na Kujadili leo Sudan na Somalia, viongozi wa Umoja wa Afrika, jana pia walizungumzia hali ilivyo nchini Misri na kumtaka Rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak kuitikia kilio cha waandamanaji hao.
Kuhusiana na mzozo wa Cote d'Ivoire, Umoja wa Afrika ulikubaliana kuanzisha tume itakayowajumuisha viongozi watano wa nchi, ili kuweza kuupata ufumbuzi mzozo wa kisiasa nchini hmuo katika kipindi cha mwezi mmoja, hatua ambayo inaondoa kitisho cha matumizi ya nguvu.
Aidha mkutano huo pia ulimchagua Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang, kuwa mwenyikiti mpya wa umoja huo wenye wanachama 53.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed