1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Paris wajadili fursa na vitisho vya akili mnemba

10 Februari 2025

Mkutano wa kilele unaojadili fursa na vitisho vya teknolojia inayokua kwa kasi ya akili mnemba umeanza rasmi Jumatatu (10.02.2025) mjini Paris na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi karibu 100 na wadau wengine.

https://p.dw.com/p/4qHDk
Mkutano wa kilele kuhusu teknolojia ya akili mnemba wafanyika Paris, Ufaransa
Mkutano wa kilele kuhusu teknolojia ya akili mnemba wafanyika Paris, UfaransaPicha: Eliot Blondet/abaca/picture alliance

Mkutano huo kuhusu akili mnemba utajikita kwanza katika suala muhimu la uwekezaji katika teknolojia hiyo hasa wakati huu mataifa na makampuni yakijitahidi kukabiliana na urasimu ambao wamesema unapelekea ufanisi mdogo.

Mkutano huo wa kilele wa Paris umeandaliwa kwa pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, na unalenga kuweka msingi imara kwa sekta hiyo changa, huku mataifa yenye nguvu duniani yakishindana ili kuwa vinara wa teknolojia hiyo.

Miongoni mwa viongozi wakuu wanaohudhuria kongamano hilo la akili mnemba mjini Paris ni pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Makamu Waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na wengine wengi.

Mkutano wa AI mjini Paris
Mkutano kuhusu akili mnemba (AI) mjini ParisPicha: Eliot Blondet/abaca/picture alliance

Akihutubia mkutano huo katika ukumbi wa "Grand Palais" mjini Paris, mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) amesema teknolojia ya  akili mnemba  inahatarisha kuzidisha tofauti za kijinsia badala ya kusababisha kitisho kwa ajira zote ulimwenguni. Gilbert Houngbo amesema kwa sasa, AI inachukua kwa njia isiyo sawa nafasi nyingi za watu katika kazi za ukarani zinazoshikiliwa na wanawake.

Viongozi mbalimbali wanakutana pia pembezoni mwa mkutano huo ambapo kesho Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anatarajiwa kukutana na Makamu wa rais wa Marekani JD Vance huku Macron akimkaribisha siku ya alhamisi kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohamed Bin Zayed al Nahyan.

Ushindani katika teknolojia ya akili mnemba (AI)

Wakati Rais wa Marekani Donald Trump akiondoa vizuizi vyote vilivyowekwa na mtangulizi wake kuhusu matumizi ya akili mnemba AI, akisema ni kwa dhamira ya kulinda na kukuza ushindani wa Marekani, shinikizo limekuwa likiongezeka kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya kulegeza sheria kuhusu teknolojia hiyo, ili kuyasaidia makampuni ya Ulaya kutopitwa na wakati katika suala hilo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akihojiwa kuhusu mkutano huo wa AI
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akihojiwa kuhusu mkutano huo wa AIPicha: Jacques Witt/SIPA/picture alliance

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya akiwemo mwenyeji wa mkutano huo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wanatumai kuwa kutakuwepo sheria mpya kuhusu  matumizi ya akili mnemba  ili kuwezesha mchakato wa kuanzisha makampuni mapya. Macron ametangaza pia uwekezaji wa euro bilioni 109 katika teknolojia ya AI ya Ufaransa, fedha zitakazotolea na sekta binafsi. Watu kadhaa waliandamana mjini Paris wakitaka kuwepo sheria ya kuidhibiti teknolojia hiyo. Maxime Fournes ni mmoja wao:

"Tunaiogopa AI kwa sababu wataalam wameeleza kwa miaka mingi kwamba hii ndiyo teknolojia hatari zaidi kuwahi kubuniwa, na ambayo inaweza kwa muda mfupi kuutokomeza ubinadamu. Sasa tunazungumzia muda wa miezi na sio tena miaka."

Hata hivyo, wachambuzi wanasema katika mkutano huo wa Paris itakuwa vigumu kupatikana makubaliano yatakayoafikiwa na pande zote hasa ikizingatiwa kuwa Umoja wa Ulaya, Marekani, China na India, zina vipaumbele tofauti katika masuala ya maendeleo na udhibiti wa teknolojia hii ya akili mnemba.

(Vyanzo: Mashirika)