1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa EU waingia siku ya tatu

19 Julai 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatana kwa siku ya tatu kujaribu kufikia makubalino ya mpango mkubwa wa kufufua uchumi wa baada ya janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3fXpf
EU-Sondergipfel zur Bewältigung der Corona-Wirtschaftskrise
Picha: picture-alliance/dpa/AP Pool/F. Seco

Viongozi wa kanda hiyo wamesalia kwenye mkwamo kuhusu mpango huo wa uokozi wa baada ya janga la COVID-19 kufuatia upinzani kutoka mataifa yanayotajwa kuwa "bahili" yakiongozwa na Uholanzi pamoja na washirika wake Austria, Denmark, Finland na Sweden

Baadaye leo rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel anatarajiwa kuwasilisha pendekezo jingine kwa viongozi wakuu 27 wa nchi wanachama baada ya mpango wake wa Euro bilioni 750 kukataliwa na mataifa tajiri ya kanda hiyo.

Mapendekezo mapya yatapunguza kidogo kiwango kilichotengwa kwa ajili ya misaada na kuongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya mikopo inayopaswa kurejeshwa na mataifa yatakayonufaika na mpango wa uokozi.

EU-Sondergipfel zur Bewältigung der Corona-Wirtschaftskrise
Rais wa Baraza la Ulaya Charles MichelPicha: picture-alliance/dpa/AP/Reuters Pool/F. Lenoir

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesisitiza kuwa mataifa wanachama wabaki na uamuzi wa mwisho wa ufadhili wowote – ikiwa ni kama kura ya turufu – kwa wapokeaji.

Pia anasema usimamizi wa Umoja wa Ulaya ni muhimu kuzilazimisha nchi kama vile Uhispania na Italia kuufanyia mageuzi uchumi wao ili kukabiliana vyema na migogoro ya usoni.  

Duru ya kidiplomasia ya Ufaransa imesema Rais Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walikataa shinikizo la Rutte na washirika wake la kupunguza misaada katika mpango huo hadi chini ya euro bilioni 400.

Pendekezo hilo lilitolewa katika mkutano ambao uliwaleta pamoja Macron na Merkel dhidi ya Rutte na viongozi wengine wa kundi lake la washirika linalofahamika kama "Frugal Five” – Austria, Denmark, Sweden na Finland.

Wakati huo huo Rais wa Benki ya Dunia David Malpass ametoa wito wa mpango wa kusimamishwa madeni ya nchi maskini zilizoathirika na virusi vya corona kurefushwa hadi mwishoni mwa mwaka wa 2021 huku mashirika kadhaa ya hisani yakisema unapaswa kurefushwa hadi 2022 ili kuepusha janga kwa mamia ya mamilioni ya watu.

Katika taarifa yao ya mwisho baada ya mazungumzo kwa njia ya video yaliyoongozwa na Saudi Arabia, mawaziri wa nchi za G20 na wakurugenzi wa mabenki walisema watazingatia uwezekano wa kurefusha mpango wa kusimamishwa madeni katika nusu ya pili ya mwaka wa 2020.

Mpaka sasa, nchi 42 zimewasilisha maombi kwa ajili ya mpango huo, zikiomba deni la pamoja la dola bilioni 5.3 kuahirishwa.

afp, ap