1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 umemalizika Los Cabos

20 Juni 2012

Viongozi wa G20 wameshadidia umuhimu wa kuharakisha ukuaji wa uchumi na kuepukana na mitindo ya kujipendelea.Mgogoro wa kanda ya Euro ndio uliogubika majadiliano katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili.

https://p.dw.com/p/15IGb
Nembo ya mkutano wa kilele wa G20-Los Cabos MexicoPicha: AP

Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa-IMF, Christine Lagarde amefurahishwa na ahadi za fedha zilizotolewa,japo kama si moja kwa moja kwaajili ya kanda ya Euro,lakini zinaweza kutumika ili kuzisaaidia nchi zinazotumia sarafu ya Euro.Dola bilioni 456 za kimarekani zitatumiwa na shirika la fedha la kimataifa kukabiliana na migogoro.

Katika taarifa ya mwisho,mataifa ya kanda ya Euro yameahidi "kuchukua hatua zote zinazohitajika" ili kudhamini utulivu na mshikamano katika eneo hilo pamoja na kuhakikisha masoko ya hisa yanafanya kazi ipasavyo.

"Mbolea nchi za Ulaya inayoihitaji kwaajili ya kuoteshea mbegu zake,imepatikana Los Cabos..."Amesema mkuu wa shirika la fedha la kimataifa Chrstine Lagarde.

Los Cabos G20 Gruppenbild
Picha ya pamoja ya viongozi wa G 20Picha: AP

Hata rais Barack Obama wa Marekani amezisifu nchi za Ulaya kwa juhudi zao:

"Hakuna shaka yoyote,nchi za Ulaya zinatambua kwamba mikakati ya kuinua uchumi ni muhimu na zinabidi zifuatane na mipango ya kuimarisha bajeti"

Kuhimiza ukuaji wa uchumi na wakati huo huo kudhamini utulivu wa bajeti-ni utaratibu unaofaa pia kwa Marekani amesema rais Barack Obama.Ameelezea matumaini yake kuziona nchi za Ulaya zikifanikiwa kusawazisha mgogoro uliopo akihoji kanda ya Euro ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kiuchumi ulimwenguni.

Viongozi wa G20 wanasubiri hivi sasa mkutano wa baraza la Ulaya utakaofanyika June 28 hadi 29 mjini Bruxelles-mkutano unaotarajiwa kuamua juu ya muongozo unaohitajika kukabiliana ipasavyo na mgogoro wa fedha.

Matokeo ya uchaguzi nchini Ugiriki yamewapa nguvu wanaopigania sarafu ya Euro .

Merkel Los Cabos, Mexiko G20
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Kabla taarifa ya mwisho kutangazwa kansela Angela Merkel alisema mjini Los Cabos ulimwengu unaihitaji "Ulaya":

"Nnaposema Ulaya zaidi ,hapo tunazungumzia kwa mfano taasisi ya Ulaya itakayokuwa na jukumu la kusimamia shughuli za benki.Tunazungumzia juu ya hatua zaidi za ukuaji wa kiuchumi na kupitishwa muongozo kuhusu jinsi ya kufanyiwa marekebisho shughuli za benki."

Kwa jumla mkutano wa siku mbili wa kilele G-20 huko Los Cabos unataajikana umefana.

Mwandishi: Bergmann Christine/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef