1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20-G7 Washington

Saumu Ramadhani Yusuf14 Aprili 2011

<p>Mawaziri wa fedha wa nchi zenye nguvu duniani wanakutana kuanzia Alhamisi huko Washington Marekani,kujadiliana kuhusu kupanda kwa bei ya Mafuta, na hatma ya Japan kiuchumi.

https://p.dw.com/p/10te3
Mawaziri wa Fedha wa nchi za G20 mjini WashingtonPicha: AP
Mawaziri wa kundi la G7 pia wanakutana katika kikao cha faragha  kutathmini uharibifu wa kiuchumi uliosababishwa na tetemeko la ardhi nchini Japan pamoja na vuguvugu la kudai demokrasia lililosambaa katika nchi za Kiarabu.

Mawaziri wa kundi la G20 la nchi zilizoendelea na zinazoinukia  kiuchumi duniani wanakutana kuanzia jana usiku nchini Marekani kuutia msukumo mpango wa kuimarisha zaidi uchumi mpango ambao utakabiliana na msukosuko wa kiuchumi ulioikumba duniani katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo hakuna kundi hata moja linalotegemewa kutoa taarifa ingawa mawaziri wa kundi la G20 wanasubiriwa hii leo kukamilisha mkutano wao na kuelezea maafikiano yao katika kikao hicho.

G20 limekuwa kundi muhimu katika kutafuta  njia za kuhakikisha kwamba msukosuko wa fedha wa mwaka 2007 hadi 2009 haujirudii tena. Msukosuko huo ndio uliochochea  mporomoko wa kiuchumi duniani ambao haujawahi kushuhudiwa  tangu vita vya pili vya dunia.

Mwaka 2009 viongozi wa kundi hilo la G20 walikubaliana  kupunguza hali ya kutokuwepo usawa kati ya mataifa tajiri yanayouza bidhaa nje kama vile China na nchi zinazozongwa na madeni  ikiwemo Marekani ambayo wanauchumi wamekuwa wakiilaumu kwa kuchangia msukosuko huo.

Lakini wakati nchi hizo kubwa kiuchumi zikiendelea kujikwamua kutoka kwenye mgogoro huo wa kiuchumi,kundi hilo limekuwa likijikuta likiendelea kukabiliwa na hali ngumu katika kupata mwafaka juu ya hatua kamili inayoweza kuchukuliwa kuondoa hali hiyo ya kutokuwepo usawa wa kibiashara.Katika mvutano wa suala hilo Marekani na China ndizo zinazoangaliwa zaidi ingawa pia Ujerumani na Uingereza zinaweza kunyooshewa kidole.

Shirika la fedha duniani IMF ambalo linafanya kikao chake cha kila mwaka mwishoni mwa wiki hii, limelionya kundi hilo la G20 kutojiweka nyuma katika kuchukua hatua madhubuti kuimarisha uchumi kwasababu ya kuona kwamba makali ya mgogoro wa kiuchumi yamepungua.

Shirika la IMF limesema kwamba ili nchi hizo ziweze kuimarisha uchumi zaidi zinalazimika kukabiliana kwanza na nakisi zake za bajeti.Shirika hilo limesababisha mjadala mkubwa mapema wiki hii liliposema kwamba Marekani huenda ikawa na kibarua kigumu kufikia lengo la kundi la G20 la kutaka kupunguza kwa nusu nakisi ya bajeti kufikia mwaka 2013.Waziri wa Fedha wa Marekani Timothy Geithner amesisitiza kwamba nchi yake itafikia malengo hayoRais Obama ameshatangaza mpango wake wiki hii wa kupunguza nakisi ya bajeti ya Marekani kwa Trillioni 4 katika kipindi cha Miaka 10.

Aidha mkutano huo wa Washington pia utazungumzia masuala ya sarafu na mageuzi ya mfumo wa shirika hilo la fedha duniani IMF.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri AbdulRahman.