1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkenya akamatwa baada ya kuikosoa Qatar

18 Mei 2021

Kijana raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 28 Malcolm Bidali hajulikani aliko baada ya kukamatwa na vikosi vya usalama vya Qatar baada ya kuandika simulizi ya kukosoa mazingira ya kufanya kazi nchini humo

https://p.dw.com/p/3tZ15
Katar
Picha: picture alliance/dpa/V.Melnikov

Raia wa Kenya aliyeandika matukio ya hali ya ukiukaji wa haki za binadamu na changamoto zinazowakabili watu wanaoishi kama wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya kiwango cha chini nchini Qatar, amekamatwa chini ya mazingira yasiyoeleweka katika taifa hilo lenye utajiri wa nishati ya mafuta.

Mkenya huyo, Malcolm Bidali, alikuwa akipigania haki zao kama wafanyakazi wa kigeni nchini humo. Kukamatwa kwake kumeibua upya harakati za kumulika suala zima la kikomo cha uhuru wa mtu kujieleza katika nchi hiyo itakayoandaa michuano ya FIFA ya Kombe la Dunia la Soka mnamo mwaka 2022.

Tukio hilo pia linaonesha changamoto zinazowakabili wafanyakazi wengi wa kigeni pale wanapokubali kuchukua fursa ya kufanya kazi katika mataifa ya Kiarabu ya Ghuba, kazi za kuingia kwa zamu ambazo zinawahitaji kufanya kwa masaa mengi.

Wafuasi wa Mkenya huyo wanasema kwamba vikosi vya usalama vya Qatar vilimkamata Bidali mnamo Mei 4 jioni na hadi sasa hawajatoa taarifa yoyote kuhusu aliko.

Katar Öl- und Erdgasförderung bei Ras Laffan
Picha: Getty Images/AFP/K. Jaafar

Serikali ya Qatar ilipohojiwa  siku ya Jumanne na shirika la habari la Associated Press ilisema kwamba Bidali amewekwa rumande na uchunguzi unafanyika kuhusu tuhuma za kumhusisha na ukiukaji wa sheria na kanuni za usalama za nchi hiyo.

Hata hivyo, serikali hiyo ilikataa kutoa maelezo kuhusu hasa kilichomfanya akamatwe na wapi anakozuiliwa na ikiwa amepata msaada wowote wa kuwasiliana na ubalozi wake, pamoja na kutambulishwa mashtaka ambayo yanaweza kumkabili.

James Lynch, mkurugenzi wa shirika la utafiti na miradi linalotetea wafanyakazi wa kigeni katika nchi za Mashariki ya kati la FairSquare lenye makao yake mjini London - Uingereza, amesema Qatar imechukua hatua nyingi za kuleta mabadiliko katika mifumo yake ya ajira, lakini wakati anapojitokeza mfanyakazi wa kigeni kuzungumza kuhusu uzowefu wake nchini humo kama mfanyakazi wa kigeni na kutowa mwito wa mabadiliko kwa njia ya amani, kinachoonekana ni kunyamazishwa kwa mfanyakazi huyo na kupotezwa.

Bidali ni kijana wa miaka 28 aliyekuwa akifanya kazi kwa muda wa saa 12 kwa siku kama mlinzi na katika muda wake wa mapumziko alikuwa akiandika kupitia jina alilotumia na NOAH kuhusu anachopitia nchini humo kama mlinzi, ikiwemo kujaribu kuimarisha mazingira anayoishi aliyopewa na muajiri wake.

Hali aliyokuwa anaieleza kwenye simulizi yake wakati mwingine alikuwa akiisifia Qatar kama nchi ya mfano katika maeneo mengi.

Katar Gastarbeiter aus Ghana in Doha
Picha: Getty Images/AFP/M. Naamani

Hata hivyo hakuwa na kigugumizi katika kuelezea hali ya mbaya ya msongamano kwenye vyumba vya kulala ambavyo walikuwa wakitumia pamoja na wenzake.

Baadhi ya vyumba walilala hadi watu 10 chumba kimoja na wakati mwingine alikuwa akieleza hata namna ambavyo wanashindwa kupata kile alichokiita ''anasa ya kuwa na faragha'', ambayo wanaipata wafanyakazi wa maofisini kutoka nchi za Magharibi walioko Qatar au hata wazawa wenyewe.

Katika simulizi yake moja, Mkenya huyo  anayeshikiliwa na vikosi vya usalama vya Qatar ameuliza: ''Kwanini suala la kuwa na mpenzi wako au hata familia yako liwe linapaswa tu kuwahusu raia waliobahatika na wenye fedha?"

Kisa cha kukamatwa Bidali hakijulikani ingawa siku kadhaa kabla ya tukio hilo alizungumza kwenye mkutano wa video na mashirika ya kiraia na mashirika ya kutetea wafanyakazi ambapo alionekana akizungumzia aliyowahi kupitia.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef