Mji wa Gaza washambuliwa vibaya na Israel
17 Mei 2021Ndege za kivita za Israel zimeshambulia katika maeneo mengi ya mji wa Gaza leo asubuhi. Mashambulizi ya silaha nzito yamefanyika kutoka kaskazini hadi kusini mwa mji huo kwa muda wa dakika 10 na uharibifu mkubwa umetokea.
Miripuko mizito iliutetemesha mji wa Gaza mapema kabisa leo Jumatatu na inaelezwa kwamba mashambulizi hayo ya anga yalikuwa makubwa, yaliyofanywa katika sehemu kubwa ya mji huo na yalichukua muda mrefu zaidi kuliko yale yaliyotokea saa 24 kabla ya hapo, ambapo Wapalestina 42 waliuwawa.
Mashambulizi hayo yalikuwa ndiyo ya umwagikaji mkubwa wa damu katika duru hii ya machafuko baina ya Israel na kundi la Hamas linaloitawala Gaza. Jeshi la ulinzi la Israel, IDF, katika taarifa yake fupi limesema limeharibu kilomita 15 za njia za chini kwa chini na makaazi ya makamanda tisa wa Hamas. Limesema mashambulizi yake ya anga yanayalenga maeneo yanayokaliwa na magaidi peke yake katika ukanda huo wa Gaza.
Ripoti zinaonesha kwamba mashambulizi hayo ya Israel kwenye mji wa Gaza yameyaporomosha kabisa majengo matatu na kiasi watu 42 waliuwawa jana Jumapili.
Mwandishi habari wa shirika la AP ameyanasa matukio ya kutisha yanayoonesha dakika za mwisho za kuondoka kwenye ofisi yao ya Gaza kabla ya ofisi hiyo kuripuliwa na wanajeshi Waisrael. Jengo mojawapo lililoshambuliwa na wanajeshi hao ndimo ilimokuwemo ofisi ya shirika la habari la Associated Press katika Ukanda huo wa Gaza,licha ya shirika hilo kutoa ombi la dharura la kuzuia mashambulizi hayo.
Mhariri mwandamizi wa shirika hilo ametowa mwito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya shambulizi hilo. Maandamano yamefanyika katika miji kadhaa mikubwa ya Marekani na waandamanaji wameitaka Israel isitishe mashambulizi katika Ukanda huo wa Gaza.Ama nchini Ufaransa polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuyazima maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yaliyopigwa marufuku mjini Paris.Lakini pia Maandamano yalishuhudiwa Jumapili katika mitaa ya mji mkuu wa Morrocco, Rabat, ambako waandamanaji walikusanyika nje ya majengo ya bunge.
Maandamano yalishuhudiwa pia katika miji mingine ikiwemo katika mji wa Casablanca mji mkubwa kabisa nchini Morrocco ambako waandamanaji walisikika wakiimba nyimbo za kulaani vitendo vya jeshi la Israel.Morroco ni moja ya nchi za kiislamu,iliyorudisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka jana.
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limeshindwa hadi sasa kutoa tamko kuhusu machafuko hayo baada ya vikao vyake viwili vya ndani mnamo siku ya Jumatatu na Jumatano wiki iliyopita. Kikao cha kwanza cha wazi kilichofanyika jana Jumapili pia kimeshindwa kutoa tamko.
Nchi wanachama wa baraza hilo zimeshindwa kuishawishi Marekani kuunga mkono tamko la kulaani machafuko hayo. Mabalozi wa China, Norway na Tunisia kwa pamoja waliamua kutoa tamko lao kuhusu Gaza,wakitaka kusitishwa mara moja kwa matumizi ya nguvu,uchokozi na uharibifu.
Wakati huo huo shirika la waandishi habari wasiokuwa na mipaka lenye makao yake Paris Ufaransa limeitaka mahakama ya kimataifa inayoshuhughulikia kesi za uhalifu wa kivita kuchunguza mashambulizi yaliyofanywa na Israel dhidi ya ofisi 23 za mashirika ya habari ya kimataifa na ya ndani katika kipindi cha siku sita.
Katika Umoja wa Ulaya mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Josep Borrell amesema mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama wa umoja huo watakutana Jumanne kesho kuzungumzia kile kinachoweza kufanywa na jumuiya hiyo kumalizika machafuko ya Israel na Wapalestina.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef