1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Bor kukombolewa mikononi mwa waasi?

8 Januari 2014

Serikali ya Sudan Kusini imesema iko tayari kuukomboa tena mji wa Bor kutoka mikononi mwa waasi, huku mazungumzo ya kurejesha amani yakionekana kwenda taratibu mjini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/1AmtF
Zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia makaazi yao.
Zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia makaazi yao.Picha: Reuters

Madai hayo yamekuja kukiwa na taarifa za kuendelea kwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu, huku mashirika ya misaada yakionya kutokea kwa mripuko wa magonjwa.

Moja ya mashirika hayo, la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka, limeonya kuwa watu waliokimbia makaazi yao wapo hatarini kupata magonjwa, huku kukiwa na ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa maelfu ya watu wanaendelea kuyakimbia makaazi yao kila siku, huku vijiji vingi vikiteketezwa kwa moto.

Jeshi la Sudan Kusini limesema liko mbioni kuukomboa mji mkuu wa jimbo la Jonglei, Bor, na kwamba serikali imetawanya wanajeshi wake katika maeneo yote yaliyopo karibu na mji huo, kaskazini mwa mji wa Juba.

Hata hivyo msemaji huyo wa waasi, Moses Ruai Lat, ameyaita madai hayo kuwa propaganda , huku akisisitiza kuwa hakuna matatizo yoyote kwa sasa.

Rais wa Sudan ,Omar al-Bashir na Salva Kiir wa Suda Kusini wakiwa mjini Juba.
Rais wa Sudan ,Omar al-Bashir na Salva Kiir wa Suda nKusini wakiwa mjini Juba.Picha: Reuters

Kikao cha mazungumzo ya amani chaahirishwa

Huku hayo yakiendelea wawakilishi kutoka pande zote mbili yaani serikali na waasi wanaendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kusitishwa mapigano mjini Ethiopia, Addis Ababa, ingawa kikao kilichokuwa kimepangwa kufanyika asubuhi hii kimeahirishwa kufuatia wawakilishi wa serikali kurejea mjini Juba kwa mashauriano zaidi na Rais Salva Kiir.

Msemaji wa waasi kwenye mazungumzo hayo, Hussein Mar, amesema kuwa kwa sasa kuna maendeleo kwa kuwa hakuna kutofautiana na kwamba mazungumzo ya amani yataendelea tena hapo kesho.

Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Jumuiya ya Ushirikiano ya nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, yanalenga kutafuta muafaka wa kumaliza mapigano hayo yaliyodumu kwa wiki tatu sasa.

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamethibitishwa kuwa zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine 200,000 wamewachwa bila makaazi tangu kuzuka kwa mapigano hayo Desemba 15 mwaka jana, wakati Rais Salva Kiir alipoyatuhumu majeshi yanayomuunga mkono aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwa kujaribu kufanya mapinduzi, jambo ambalo limekanushwa na Machar

Jeshi la Sudan Kusini kuukomboa mji wa Bor.
Jeshi la Sudan Kusini kuukomboa mji wa Bor.Picha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Suala kubwa kwa sasa kutoka kwa waasi na jumuiya za kimataifa ni kuitaka serikali ya Sudan Kusini kuwaachia maafisa 11 walio karibu na Machar ili waweze kushiriki mazungumzo ya amani, jambo ambalo halijapatiwa muafaka.

IGAD imewatuma wajumbe wake kwenda Juba kumshinikiza Rais Salva Kiir kuwaachia wafungwa hao wa kisiasa, suala ambalo upande wa waasi unataka ili mazungumzo yalete maana.

Mwandishi: Flora Nzema/AFP/IPS

Mhariri: Mohamed Kehelef