1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri na Iraq zazidi kuimarisha mahusiano yao

5 Machi 2023

Waziri mkuu wa Iraq Mohammed Shia-al Sudani akutana na rais wa Misri Abdul-Fatah Al Sissi mjini Cairo katika hatua ya kuonesha mshikamano zaidi wa mahusiano

https://p.dw.com/p/4OH1s
Ägypten | Präsident Abd al-Fattah as-Sisi
Picha: Ahmad Hassan/AFP/Getty Images

Rais wa Misri Abdel Fattah al Sissi amefanya mazungumzo leo Jumapili na waziri mkuu wa Iraq mjini Cairo wakati nchi hizo mbili zikiimarisha mahusiano yao na kuongeza nguvu ya mshikamano wa kikanda pamoja na Jordan.

Mohamed Shiaa Al-Sudani | im DW Interview
Picha: DW

Waziri mkuu wa Iraq Mohammed Shia-al Sudani aliwasili Cairo na kupokelewa katika uwanja wa ndege na mwenzake Mustafa Mabouly,na kwa pamoja wakapata fursa ya kukagua gwaride la heshima lililocheza wimbo wa mataifa hayo mawili.

Baadae waziri mkuu huyo alikutana na rais Al Sissi ikulu ya mjini Cairo ambako walijadili kuhusu masuala ya ushirikiano wa kiuchumi na usalama baina ya nchi zao,kwa mujibu wa msemaji wa ofisi ya rais wa Misri Ahmed Fahmy.

Kadhalika walijadili juu ya masuala ya kikanda ikiwemo ushirikiano na Jordan kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa ingawa hakuna ufafanuzi zaidi uliowekwa wazi. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje na biashara wa nchi zote mbili Misri na Iraq.

Ziara ya kiongozi huyo wa Iran nchini Misri ni ya kwanza tangu baraza lake la mawaziri lilipoidhinishwa  na bunge la Iraq mnamo mwezi Oktoba mwaka jana na kumaliza mkwamo wa kisiasa uliodumu mwaka mzima nchini humo.

Itakumbukwa kwamba mtangulizi wake waziri mkuu huyo wa Iraq, Mustafa al Kadhimi alitengeneza ushirikiano wa karibu na El Sisi pamoja na mfalme Abdulla wa pili wa Jordan.Mgogoro wa kisiasa wazidi kutanuka Iraq

Jordanien Nahost-Gipfel in Amman | Mohamed Shia al-Sudani
Picha: Yousef Allan/Jordanian Royal Palace/AFP

Na mwaka 2021 rais El Sissi alikwenda Baghadad akiwa ni kiongozi wa kwanza wa juu wa nchi kuwahi kuitembelea Iraq tangu miaka ya 1990,baada ya mahusiano kati ya nchi hizo mbili kuharibika vibaya kufuatia uvamizi uliofanywa nchini Kuwait na rais wa Iraq wa wakati huo Saddam Hussein. Misri,Iraq na Jordan zimeongeza mahusiano yao na viongozi wa nchi hizo wameshakutana mara tano kwa mikutano ya kilele tangu mwaka 2019.

Iraq hivi karibuni iliandaa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia yakilenga kujaribu kuzileta pamoja nchi hizo mbili mahasimu wa jadi wa kikanda kurekebisha mahusiano yao lakini pia kuutazama mgogoro wa Yemen.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW