Misaada zaidi yaingizwa Gaza baada ya kusitishwa mapigano
24 Januari 2025Tukianza kuangazia masuala ya kiutu, Shirika la Kimataifa la Huduma za Kiutu, OCHA limearifu hii leo kwamba malori 653 yameingia Ukanda wa Gaza kupitia mipaka ya Erez na Zikim kaskazini mwa eneo hilo, pamoja na mpaka wa Kerem Shalom, uliopo kusini mwa Gaza. OCHA, limenukuu taarifa hizo kutoka kwa mamlaka za Israel na waratibu wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
Shirika hilo limesema, wafanyakazi wa misaada na wale wanaojitolea sasa wanaweza kufikia maeneo ambayo hapo kabla yalikuwa ni vigumu kuyafikia na kuongeza kuwa mazingira ya kiutendaji yameimarishwa kwa kiasi kikubwa. Kwa ujumla mashirika ya misaada kwa sasa yanafikisha huduma za kiutu kwenye maeneo mengi zaidi.
Msaada mkubwa zaidi ulioingizwa Gaza tangu makubaliano hayo yalipoanza kutekelezwa ni vyakula. Vifaa kama dawa, tiba, vifaa kwa ajili ya makazi, usafi na maji vinatarajiwa kufika siku chache zijazo.
Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanajumuisha ufikishwaji wa misaada kwa haraka kwa zaidi ya watu milioni 2 wa Gaza, ambao asilimia 90 miongoni mwao wameathirika pakubwa na njaa, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.
Lakini katikati ya haya, yapo mashaka kwamba juhudi za umoja huu zinaweza kuathirika kutokana na upungufu wa ufadhili. Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu kwenye Maeneo yanayokaliwa kimabavu ya Palestina Muhannad Hadi, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanahitaji fedha haraka ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kutoa msaada kwa siku 42, lakini pia baada ya siku 42, kwa sababu wana matumaini kwamba watatoka awamu ya kwanza hadi ya pili.
Watoto walia "ulimwengu umewageuzia mgongo"
Katika hatua nyingine, OCHA imesema vita katika Ukanda wa Gaza vimesababisha maumivu makubwa kwa watoto ambao miongoni mwao wamekufa ama kwa mashambulizi au hali mbaya ya hewa kama baridi kali. Wengine wameathiriwa na njaa na wengine wakibaki yatima ama kutenganishwa na familia zao.
Mratibu wa shirika hilo Tom Fletcher amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa na Urusi jana Alhamisi kwamba, kizazi hicho kinapitia wakati mgumu. Amesema, makadiro yanayonyesha zaidi ya watoto 17,000 wametenganishwa na familia zao.
Soma pia:Watoto 7 wamekufa kwa baridi kali Gaza huku makumi wakiuawa
Fletcher amesema "Watoto wa Gaza wasilengwe kwa makusudi. Wanastahili kuishi kama watoto wengine kwa usalama, kupata elimu na kuwa na matumaini. Wanatuambia, ulimwengu haukuwepo kwa ajili yao katika muda wote wa vita hivi. Ni lazima tuwepo kwa ajili yao sasa.”
Hata hivyo, Fletcher hakutoa takwimu zozote za vifo vya watoto, ingawa alisema, wengine walikufa hata kabla ya kuvuta pumzi yao ya kwanza, wakati mama zao waloaga dunia wakati wanazaliwa. Karibu wanawake 150,000 wajawazito pamoja na wazazi pia wapo kwenye mashaka makubwa kutokana na kukosa huduma za kiafya.
Shirika la Kuwahudumia watoto la umoja huo, UNICEF limesema watoto wa Gaza wanahitaji msaada wa kisaikolojia, tiba za afya ya akili ili pamoja na mambo mengine kuwanusuru na wasiwasi na mawazo ya kujiua.
Jenin bado kunafukuta
Mbali na masuala ya kiutu, taarifa kutoka Jenin na Tel Aviv zinasema jeshi la Israel jana Alhamisi liliwaua Wapalestina wawili waliojihami kwa silaha katika mji wa Jenin wakati jeshi hilo likiendesha operesheni yake kubwa kwenye mji hio uliopo kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
Limesema, wanaume hao waliuawa kufuatia mabadilishano ya risasi, ambapo mwanajeshi wa Israel alijeruhiwa. Limesema wanaume hao walikuwa ni wanamgambo wa kundi la Palestinian Islamic Jihad, PIJ. Lakini baadae, kundi la Hamas kupitia tawi lake la kijeshi la al-Qassam lilisema walikuwa ni wapiganaji wake.
Soma pia: