1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikutano ya kilele isiyojulikana tija

Oumilkheir Hamidou
3 Desemba 2018

Mkutano wa kilele wa mataifa 20 yaliyoendelea na yanayoinukia kiviwanda G-20 mjini Buenos Aires, mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi mjini Kattowitz na ghadhabu za vizibao vya manjano nchini Ufaransa magazetini.

https://p.dw.com/p/39JXr
UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen
Picha: Reuters/K. Pempel

 

Tunaanzia Buenos Aires ambako mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia umemalizika bila ya matokeo ya maana kufikiwa. Hata taarifa ya mwisho si bayana. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika:"Cha maana pekee ni ile hali kwamba taarifa ya mwisho ya mkutano huo wa G-20 imeweza kutolewa. Haina ufafanuzi lakini. Kwa hivyo hakuna cha kujitenganisha nayo. G-20 ni jumuiya inayowakilisha thuluthi mbili ya wakaazi wa dunia na robo tatu ya biashara ya dunia. Lakini hakuna tatizo lolote lililotatuliwa. Ulikuwa mkutano wa kilele wa mitihani na watu kuvunjika moyo."

Mbio za sakafuni

Gazeti la "Westfalen-Blatt" linautaja mkutano wa kilele wa G-20  kuwa ni "mbio za sakafuni". Gazeti linaendelea kuandika: "Usumbufu wa Kansela Angela Merkel kuelekea Argentina mtu anaweza kusema unalingana na jinsi mkutano wenyewe wa kilele wa G-20 ulivyokuwa. Ghasia tu hakuna chochote cha maana kilichopatikana. Labda makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na China ya kusaka ufumbuzi wa mzozo wa kibiashara kati yao ndio tukio pekee la maana la mkutano huo."

Uhusiano kati ya madola makuu ndio chanzo cha kufanikiwa au la juhudi za kimataifa

Mkutano mwengine wa kilele umefunguliwa nchini Poland. Unahusiana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake. Mkutanao huo uliofunguliwa leo unafanyika katika mji wa migodi ya makaa mawe wa Kattowitz. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linamulika mkutano huo na kuandika: "Hali ya kisiasa namna ilivyo duniani inafifiisha matumaini yote watu waliyojiwekea. Madola makuu hayana msimamo mmoja, kama ilivyoshuhudiwa mwishoni mwa wiki katika taarifa ya mwisho ya mkutano wa kilele wa G-20. Wanakosa nia ya kufikia ufumbuzi wa pamoja wa matatiizo yanayowasumbua walimwengu. Mzozo wa madola makuu unapalilia pia mzozo wa mabadiliko ya tabianchi."

 Fujo za vizibao vya manjano Ufaransa

Machafuko ya wanaharakati wanaojiita "vizibao vya manjano" yanagonga vichwa vya habari ndani na nje ya Ufaransa. Mwishoni mwa wiki wameuvamia mtaa mashuhuri wa Champs Elysée na kuvunja vunja maduka pamoja na kuuchafua mnara wa "Arc de Triomphe" au Upinde wa ushindi". Gazeti la Badische Neueste Nachrichten" linaandika: "Emmanuel Macron hakufanikiwa kuwatanabahisha wafaransa kuhusu umuhimu wa sera zake za mageuzi. Na zaidi kuliko yote mnanmo miezi iliyopita  amezidi kulipanua pengo kati ya masikini na matajiri. Matokeo yake ni hasira za vizibao vya manjano zilizogeuka matumizi ya nguvu yaliyokithiri.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef