Miaka mitano baada ya ghasia za uchaguzi, Kenya imejifunza nini?
28 Desemba 2012Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa taifa la Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta, wanaongoza kambi mbili za upinzani.
Viongozi hawa wanaotokea makabila tofauti huku Uhuru Kenyata akitokea Kabila la Kikuyu na Raila Odinga akiwa wa Kabila la Luo, hali hiyo inaashiriria mpasuko na mabishano ya kisiasa, mabishano ambayo katika uchaguzi wa mwaka 2007 yalisababisha mauaji ya watu zaidi ya 1,200 na kuacha wengine mamia bila ya makaazi.
Mmoja wa wanaharakati aliyesaidia kutuliza ghasia mara baada ya machafuko ya uchaguzi mwaka 2007, Mzalendo Kibunjia, amesema bila ya kuongeza hisia lakini historia ya chaguzi nchini Kenya watu wa Kabila la Kikuyu na Waluo wamekuwa katika ushindani kila wakati wa uchaguzi unapofikia.
"Unachotarajia hapa ni nini? Kila mara chaguzi zetu zimekuwa katika ukabila na si demokrasia ya kweli, Kwa Afrika demokrasia ni udugu au ukabila na sio hali halisi" Alisema Kibunjia, ambaye sasa anaongozha tume ya utangamano na maridhiano ya kitaifa.
Kitendawili cha ICC na siasa za ukabila
Hali nyengine inayoelezwa kuwa itaufanya uchaguzi nchini Kenya kuwa wa wasiwasi ni mashtaka yanayomkabili Uhuru Kenyatta katika mahakama ya jinai ya Kimataifa ICC, ambapo anatuhumiwa kuhusika na mauaji wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Shaka iliyopo ni iwapo Kenyatta atashinda uchaguzi huku mashitaka yanayomkabili yakiendelea ambayo Mahakama hiyo inamtuhumu kwa kuwashawishi vijana wa kabila lake la Kikuyu kupambana na vijana wa Kabila la Waluo, na kusababisha mauaji na umwagaji damu. Hata hivyo Uhuru amekanusha mashitaka hayo.
Ili kushinda awamu ya kwanza ya uchaguzi mwezi Machi mwaka ujao mgombea anapaswa kupata ushindi mkubwa wa kura kutoka kwa wapigakura 14 nukta 3 milioni. Hakuna mgombea anayeweza kupata kura hizo, na hivyo huenda duru ya pili uchaguzi ikafanyika mwezi Aprili.
Kutokana na kura za maoni Odinga anaongoza akikaribiwa na Kenyatta hali ambayo ndiyo inayozua hofu ya kuibuka msigano wa kikabila huku kila mmoja akitaka kupata ushindi.
Aidha wapo wanaoamini kuwa mahakama ya ICC haijaelekea kutenda haki kwa viongozi wanaotuhumiwa na ambao wanawania nafasi za urais, hali ambayo itazidisha machafuko.
"Nina wasiwasi wa kuzuka kwa ghasia kama tulivyoshuhudia uchaguzi uliopita. Wakenya wamechoshwa na Mahakama ya ICC na jinsi inavyoendesha shughuli zake hapa nchini," alisema Ken Wafula anayefanya kazi na shirika la Haki eneo la Bonde la Ufa, eneo lililoshuhudia machafuko makubwa baada ya uchaguz uliopita.
Matokeo ya utafiti
Utafiti wa shirika huru la Synovate mwezi Disemba 2012 kuhusu iwapo wakenya wanaamini kama Uhuru Kenyata anaweza kuhudhuria mahakama ya ICC pale atakapokuwa rais unaonesha kuwa wengi hawaamini kuwa mgombea huyo na mwenzake William Rutto wanaweza kuhudhuria tena mahakamani.
Wachambuzi wa siasa za Kenya wanasema kuwa hata kampeni kati ya Odinga na Kenyatta zitatawaliwa na hisia za ukabila, wakionesha kuwa hata kwa wagombea kama vile Musalia Mudavadi kampeni zake zitatawaliwa na watu wa jamii ya Waluhya, ambalo ni kabila la pili lenye watu wengi nchini Kenya.
Mwandishi: Khatib Mjaj/RTRE
Mhariri: Josephat Charo