1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Mfungaji bora wa Kombe la Dunia Just Fontaine afariki dunia

1 Machi 2023

Just Fontaine, mfungaji bora wa muda wote katika kinyang'anyiro cha Kombe la Dunia akiwa na mabao 13, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89, imesema familia yake

https://p.dw.com/p/4O7Jl
Just Fontaine
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. de la Mauviniere

Fontaine aliiandika rekodi hiyo katika fainali za mwaka wa 1958 nchini Sweden ambako Ufaransa ilifika nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao, na kupoteza kwa Brazil iliyokuwa na mchezaji nyota Pele.

Akiwa sehemu ya safu ya washambuliaji watatu katika Kombe hilo la Dunia pamoja na Roger Piantoni na Raymond Kopa, Fontaine hata huenda asingekuwa Sweden.

Majeraha kwa washambuliaji wenzake Thadee Cisowski na mchezaji mwenza wa klabu ya Reims Rene Bliard yalimpa fursa ya kuwa kwenye timu ilosafiri na kisha kwenye kikosi cha kwanza.

Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps amesema "Nimehuzunishwa na habari za kifo cha Just Fontaine, kama tu ilivyo kwa wale wote wanaopenda kandanda na timu yetu ya taifa." "Justo ndiye na atabakia kuwa nguli wa Ufaransa." Amesema Deschamps.

Fontaine pia alishinda mataji manne ya Ligi ya Ufaransa, moja na Nice na matatu na timu bora ya Reims ya baada ya enzi ya vita.

Alilazimika kustaafu katika mwaka wa 1962 akiwa na umri wa miaka 28 tu baada ya kuvunjika mguu. Aligeukia ukufunzi ambapo aliifikisha Morocco katika nafasi ya tatu ya Kombe la Mataifa Afrika 1980

afp