1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mfalme Charles III kuimarisha uhusiano na Ufaransa

Sylvia Mwehozi
21 Septemba 2023

Mfalme Charles wa III wa Uingereza ameahidi kuimarisha uhusiano wa nchi yake na Ufaransa akipendekeza kuwa mataifa hayo mawili yanapaswa kuwa na ushirikiano usioyumba katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu.

https://p.dw.com/p/4WeUp
Mfalme Charles wa III mjini Paris
Mfalme Charles III wa Uingereza na Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Yoan Valat/REUTERS

Mfalme Charles amesifu mahusiano ya dhati ya Ufaransa na Uingereza na uwezo wake wa kuzikabili changamoto za ulimwengu ikiwemo vita vya Ukraine na mabadiliko ya tabia nchi, wakati alipowahutubia wabunge wa Ufaransa.

Katika siku ya pili ya ziara yake nchini Ufaransa, Charles amekutana na makundi ya wanamichezo kaskazini mwa kitongoji cha Paris na baadae atatembelea Kanisa Kuu la Notre-Dame ambalo liliharibiwa na moto.

Charles amepokelewa vyema na wabunge wa Ufaransa baada ya kuchanganya kwa ustadi lugha za Kiingereza na Kifaransa. Amewaeleza wabunge kwamba Uingereza "daima itakuwa mmoja wa washirika wa karibu na rafiki mkubwa wa Ufaransa".

Ufaransa -Mfalme Charles III
Mfalme Charles III akihutubia wabunge wa UfaransaPicha: Emmanuel Dunand/Pool/AP/picture alliance

Amesisitiza kuwa azma na muungano wa nchi hizo mbili ni muhimu zaidi "kuliko hapo awali" katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, akiongeza kuwa "Ukraine itashinda" katika vita vyake na Urusi.

"Leo, zaidi ya miaka 80 tangu tulipopigana bega kwa bega kukomboa Ulaya, kwa mara nyingine tunakabiliwa na uvamizi usio na msingi katika bara letu. Dhamira na muungano wetu ni muhimu zaidi kuliko hapo awali. Kwa pamoja, tunasimama na wananchi wa Ukraine tukiwa na mshikamano thabiti. Kwa pamoja hatuna mpinzani katika dhamira yetu kwamba Ukraine itashinda na kwamba uhuru wetu, wa thamani sana utashinda siku hiyo."

Ziara hiyo hadi hivi sasa imeripotiwa na vyombo vya habari vya nchi zote mbili kuwa ya mafanikio, huku kukiwa na kauli za hapa na pale katika mitaa ya mjini Paris za kumtakia heri Mfalme Charles.

Katika hotuba yake kwa wabunge Charles amependekeza kuwa Ufaransa na Uingereza ziunganishe nguvu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na dharura zinazovikabili viumbe hai kwa kufikia makubaliano mapya sawa na mkataba wa mwaka 1904 wa Entente Cordiale uliotia saini urafiki baina ya Paris na London.

Kauli ya Charles kuhusu ulinzi wa mazingira imetolewa siku moja baada ya waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak kulegeza sera za kijani zinazolenga kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kufikia katikati mwa karne. Ziara ya Charles ambayo ilikuwa ifanyike mwezi Machi lakini ikasogezwa mbele kwasababu ya maandamano ya umma ya kupinga mageuzi ya pensheni imetawaliwa na hafla katika taifa hilo ambalo lilikomesha utawala wa kifalme mwaka 1789 na kumuua Mfalme wake.