Merkel asikitishwa na mzozo kuhusu Maassen
24 Septemba 2018Merkel amesema ni wakati sasa wa serikali yake kuachana na mivutano na kuangazia matatizo ya watu. Hapo jana viongozi walifikiana kuwa mkuu huyo wa zamani wa shirika la ujasusi Hans Georg Maassen atakuwa mshauri maalum katika wizara ya ndani.
Masuala ambayo Wajerumani wanataka kuiona serikali ni pamoja na kuongezeka kwa kodi za nyumba, malipo ya pensheni na sakata la magari yanayotumia mafuta ya Diesel.
Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto Social Democratic-SPD kilikuwa kikisisitiza kwamba Maassen afutwe kazi kwa kushindwa kuwajibika kuhusiana na machafuko ya hivi karibuni dhidi ya wahamiaji.
Sakata hilo lilipamba moto baada ya Waziri wa ndani na kiongozi wa chama cha Christian Social union-CSU Horst Seehofer kusimama kidete kumuunga mkono na kumtetea Maassen.
Mnamo wiki iliopita , Serikali hiyo inayoongozwa na Kansela Angela Merkel kutoka chama cha Christian Democratic Union-CDU, ilikubaliana kumuondoa Maassen katika wadhifa wake na kuteuliwa kuwa waziri mdogo wa ndani, hatua ambayo ilikuwa ni kumpandisha cheo na mshahara zaidi.
Hatua hiyo ilizusha mtafaruku ndani ya chama cha SPD na kumlazimisha kiongozi wa chama hicho Andreas Nahles kutaka maafikiano hayo yajadiliwe upya.
Kutokana na mgogoro huo mpya, hatimaye pande hizo tatu CDU-CSU na SPD zikakubaliana kuwa Maassen apewe wadhifa mwengine na akateuliwa kuwa mshauri katika wizara ya ndani akiwa na jukumu la kushughulikia masuala ya Ulaya na kimataifa, huku Waziri wa ndani Seehofer akisema afisa huyo atabakia na mshahara wake ule ule wa zamani.
Kutokana na maridhiano hayo, waziri mdogo wa ndani Gunther Adler kutoka chama cha SPD atabakia katika wadhifa wake huo. Hivi sasa kiongozi wa chama hicho Nahles atalazimika kuwasilisha maridhiano hayo mapya mbele ya chama chake ili yaidhinishwe.
SPD wasema ni suluhisho muafaka
Naibu mkuu wa SPD Ralf Stegner alisema uamuzi uliofikiwa ni " suluhisho muwafaka.”
CDU na chama ndugu CSU, vimekuwa vikivutana hivi karibuni kuhusiana na suala la wahamiaji huku seehofer aliyeacha uongozi wa chama chake CSU ili kuwa waziri wa ndani akiwa na msimamo mkali kuhusu suala hilo.
Kisa cha Maassen kilianzia pale aliposema idara yake haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa wageni walikuwa wakiandamwa mitaani mjini Chemnitz baada ya mjerumani mmoja kuchomwa kisu na kuuwawa na mtu anayetuhumiwa kuwa ni mhamiaji, wakati ukanda wa video uliochapishwa kwenye mitandao ulionesha wazi wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wakiwaandama na kuwashambulia wageni mjini humo.
Mgogoro huo umegeuka mtihani kwa mustakbali wa serikali ya muungano ya Kansela Merkel katika wakati ambao vyama hivyo vitatu vinavyounda serikali hiyo, vikikabiliwa na changamoto mpya kuelekea uchaguzi wa jimbo la Bavaria wa Waziri wa ndani Seehofer Oktoba 14 na katika jimbo jirani la Hesse Oktoba 28.
Mivutano ya ndani inaelekea kudhoofisha uungaji mkono wa vyama hivyo, tokea uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwaka mmoja uliopita , ambapo chama cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia AFD kilifanikiwa kuingia bungeni na kugeuka kuwa changamoto kubwa kwa vyama hivyo asilia.
Kuna wasiwasi mkubwa kwamba matokeo mabaya kwa CSU jimboni Bavaria katika uchaguzi huo mwezi ujao yanaweza kuwa kitisho kwa mustakabali wa serikali hiyo ya muungano.
Mwandishi. Isaac Gamba/ AP, Reuters
Mhariri: Caro Robi