1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel amshutumu waziri mkuu Orban wa Hungary

Sekione Kitojo
5 Julai 2018

Kansela Angela Merkel amemshutumu kiongozi mwenye msimamo mkali wa siasa za mrengo wa kulia wa Hungary Viktor Orban kwa  kushindwa kuheshimu ubinadamu katika sera zake za uhamiaji wakati alipokutana nae mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/30uMc
Deutschland Berlin Viktor Orban und Angela Merkel
Picha: Reuters/A. Schmidt

Kansela  pia atakutana na viongozi wa  vyama  vitatu  ambavyo vinaunda  muungano  wa serikali  leo kwa mazungumzo mazito kuhusiana  na mswada  wa makubaliano ya uhamiaji  yaliyofikiwa  wiki hii pamoja  na  waziri wake muasi  wa  mambo  ya  ndani  Horst Seehofer.

Bundestag Angela Merkel und Horst Seehofer
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akimsikiliza waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer (kulia) akizungumza bungeniPicha: Getty Images/S. Gallup

Katika mpambano dhahiri kuhusiana  na  maadili  ya  ulaya  katika wakati  ambapo uhamiaji  unatishia  umoja  katika  mataifa  hayo  ya Ulaya , Merkel  na  Orban kila  mmoja  akijionesha  kuwa mtetezi mkubwa  wa lengo  la  kundi  hilo la  mataifa.  "Tatizo kama ninavyoliona, na  pale  tofauti  ilipo, ni kwamba  ni  lazima  tukumbuke kwamba  tunazungumza juu  ya  binadamu", Merkel aliwaambia waandishi  habari  katika  mkutano wa  pamoja  na  Orban.

Merkel  amesema kudhibiti  mipaka ya  Umoja  wa  Ulaya  sio kuunda ngome dhidi  ya  watu ambao  wanaletwa  na  wasafirishaji  haramu wa  watu  ama kupitia  safari  hatari  katika  jangwa  la  sahara  na bahari  ya  Mediterania. Amesema  kundi  hilo  la  mataifa  linahitaku kutia  sainia  makubaliano  na  mataifa  ya  Afrika  kuhakikisha uhamiaji  halali unawezekana.

Kwa  upande  wake  Orban  alisema  Ujerumani inapaswa  kushukuru kwa  Hungary  kujenga  ukuta katika  mipaka  yake  na  Serbia  na Croatia, ambao  alisema  unalindwa  masaa  24 kwa  siku na wanajeshi 8,000". Bila  hivyo wakimbizi 4,000  hadi 5,000 wangekuwa  wanawasili  nchini  Ujerumani  kila  siku. Huu  ni mshikamano , mshikamano  ambao unapaswa  kuchukuliwa  kwa dhati,"  amesema Orban.

Deutschland Berlin Viktor Orban und Angela Merkel
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto) akimkaribisha waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban (kulia)Picha: Reuters/A. Schmidt

Mazungumzo ya muungano wa serikali

Pia  Merkel anatarajiwa  kufanya  mazungumzo  leo  na  viongozi  wa vyama  vinavyounda  muungano  wa  serikali  yake  vya  SPD na CSU  ambapo  chama  cha  CSU kinataka  makubaliano yanayotaka kuundwe  kile  kinachoitwa  vituo vya  kuwashikilia  kwa  muda wahamiaji  karibu  na  mpaka  wa  kusini wa  Ujerumani .

Waziri  wa  mambo  ya  ndani  wa  Ujerumani  Horst Seehofer , wakati  huo  huo, anakutana  na  kansela  wa  Austria  Sebastian Kurz kufanya  majadiliano kuhusu  makubaliano ambayo yatashuhudia  Austria  ikiwarejesha  wahamiaji ambao  hawataweza kuingia  nchini  Ujerumani. Akizungumza  bungeni  leo  Seehofer alisema.

Horst Seehofer
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst SeehoferPicha: picture-alliance/A.Hosbas

"Mwanzoni mwa  wiki tulifikia  makubaliano baada  ya  mjadala  mkali katika vyama  ndugu, na  ninaamini  kabisa  kwamba  tutafikia makubaliano, serikali inayoaminika pamoja  na  mshirika  wetu chama  cha  SPD, na  hatua  muhimu  sana  hivi  sasa  ni  mpango wa  mipaka  mipya wiki  iliyopita, haikuweza  kueleweka  kwamba watu  ambao  wamepigwa  marufuku kuingia waliruhusiwa  kuingia tena  Ujerumani, kitabu  hiki  kimefungwa sasa. Tutapata vituo  vya muda  hivi  sasa  ambapo watu  wanaoomba  hifadhi  watarejeshwa kule  walikotoka katika  nchi  zile  zinazohusika  na  wao."

Merkel  amewaambia  waandishi  habari katika  mkutano na waandishi  habari  mjini  Berlin  kwamba  anataka  kulinda, ubinadamu wa  Ulaya, wakati  ikifikia  vipi  wahamiaji wanavyotendewa na  hicho ndio huenda kinatutenganisha, amesema Merkel.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga