1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Membe arejea Tanzania, asema hakukimbia kampeni

Admin.WagnerD15 Septemba 2020

Mgombea wa urais wa chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania Bernard Membe amerejea nchini humo jioni hii akitokea Dubai na kutupiilia mbali hoja kwamba alikuwa amekimbia kampeni.

https://p.dw.com/p/3iVgB
Tansania Wahl ACT Wazalendo Bernard Membe
Picha: DW/S. Khamis

Mgombea wa urais wa chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania Bernard Membe amerejea nchini humo jioni hii akitokea Dubai na kutupiilia mbali hoja kwamba alikuwa amekimbia kampeni na kwenda kujipanga nje ya nchi. Membe, mwanadiplomasia wa zamani wa taifa hilo, aliondoka nchini humo siku tano zilizopita, wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiwa zimepamba moto hali ambayo ilizusha maswali mengi. 

Mwanasiasa huyo amewasili nchini akisema kuondoka kwake ghafla hakupaswi kuchukuliwa kama ni mkakati wa kisiasa wala mpango mwingine wowote unaohusiana na uchaguzi mkuu bali alifanya hivyo kwa ajili ya kwenda kutimiza moja ya majukumu yake binafsi.

Amesema safari yake Dubai ilikuwa na malengo ya kibiashara alikokwenda kuhudhuria moja ya vikao muhimu vya kampuni aliyodai kuwa yeye ni sehemu ya wakurugenzi wake.

Tansania Beisetzung von Godfrey Dilunga
Membe, akiwa na viongozi wenzake wa chama cha ACT-WazalendoPicha: DW/S. Khamis

Kuhusu hali ya afya yake na hasa kutokana na maelezo aliyoyaandika katika akunti yake ya twitter siku moja kabla ya kurejea ,Membe amesema alitumia muda wa ziara yake kufanya uchunguzi wa kiafya jambo ambalo amedai amekuwa akilifanya mara kwa mara.

Akigeukia kuhusu mchaka mchaka wa wa uchaguzi mkuu na kampeni za urais zinazoendelea, mwanasiasa huyo aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigine wakati wa utawala wa awamu ya nne, amesema anaona hajachelewa katika kampeni.

Amedai ingekuwa jambo la kushangaza zaidi kwake na chama chake kuendelea kuzunguka na kampeni wakati sehemu kubwa ya wagombea wa ubunge na udiwani wamewekewa pingamizi na hatima yao ilikua bado haijajulikana.

Membe aliondoka nchini Ijumaa iliyopita kwa shirika la ndege la Emirate katika wakati ambapo wagombea wengine wakiwa wameanza kuimarisha kampeni zao kuelekea tarehe ya uchaguzi. Hatua hiyo ilizusha minong'ono mikubwa huku wengine wakidai huenda alienda kujipanga vyema ikiwamo kusafa fedha.

Membe amekiri kwamba vyama vya upinzani vinaingia kwenye uchauzi huu vikiwa katika hali ngumu ya kifedha, na hiyo amedai kuwa siyo kwa vyama hivyo pekee bali inawakumba pia hata wananchi wengine wa kawaida.

Wakati huu wagombea wengine wa urais wa vyama vya CCM, Chadema na CUF wakiendelea kupishana majukwaani kwa kunadi sera zao kwa wapiga kura, mgombea huyo wa ACT Wazalendo ameahidi kurejea tena kwenye majukwaa hayo Septemba 17.

Soma Zaidi: