1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kuunda serikali mpya Iraq kuanzishwa hivi karibuni

Mjahida 26 Juni 2014

Serikali ya Iraq imetangaza kuwa kikao cha bunge kitafanyika Julai mosi, ili kuanzisha mpango wa kuunda serikali mpya huku nchi hiyo ikikabiliwa na uasi unaotishia umoja wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1CQT2
Waliojitolea kuungana na jeshi la Iraq kupambana na uasi
Waliojitolea kuungana na jeshi la Iraq kupambana na uasiPicha: Reuters

Taarifa ya kuitishwa kikao hicho imetolewa na makamu wa rais Khudair al-Khuzai, ambaye ni kaimu rais kwa sasa na aliyemshirika wa karibu wa Waziri Mkuu Nouri al Maliki.

Miezi mitatu baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo sauti za kimataifa na zile za ndani ya Iraqi zimesikika zikitoa wito wa kuanzishwa mara moja mchakato wa kuundwa kwa serikali mpya.

Kwa upande mwengine kiongozi wa kidini wa madhehebu ya shia aliye na ushawishi mkubwa Moqtada al-Sadr ameapa kukabiliana na wapiganaji wa kisuni walio na siasa kali. Hatua inayotishia wasiwasi zaidi wa mapigano ya kidini katika mgogoro unaozidi kuwagawanya wairaq.

"Cha kwanza mapigano na visa vya ugaidi kwa raia ni lazima visitishwe, pili, naiomba serikali ya iraq kutimiza matakwa ya wasuni waliotengwa na kubaguliwa na tatu kuharakisha kuundwa kwa serikali ya kitaifa itakayokuwa na sura mpya itakayoyajumuisha makundi yote ya kidini nchini Iraq", Alisema Sadr.

Kiongozi wa kidini wa madhehebu ya shia Moqtada al-Sadr
Kiongozi wa kidini wa madhehebu ya shia Moqtada al-SadrPicha: ALI AL-SAADI/AFP/Getty Images

Akizungumza katika mji mtakatifu wa Najaf, Moqtada al-Sadr ameonya kuwa mataifa yote ya kigeni na yale jirani na Iraq yanapaswa kuwacha kabisa kuingilia mgogoro wa Iraq. Matamshi yake yanakuja wakati vikosi vya serikali bado vinapambana na wapiganaji wa kisunnni ambao wameyateka miji kadhaa nchini Iraq.

Kwa sasa wapiganaji watiifu kwa Moqtadar al Sadr wamesema wako tayari kupamabana na uasi nchini humo.

Wanasiasa walio na uhasama waomba kuungana dhidi ya kundi la ISIL

Wakati huo huo Waziri Mkuu Nouri al Maliki amewaonya maadui dhidi ya kuutumia mgogoro huo na kumtenga baada ya Marekani kuwasisitizia viongozi wa kisiasa walio na uhasama kuungana kupambana na kundi la kigaidi la dola la kiislamu la Iraq na eneo la Sham ISIL.

Rais wa Marekani Barrack Obama hajatoa hakikisho la kutekeleza shambulizi la angani aliloombwa kufanya na Iraq ili kukabiliana na wapiganaji wa kisuni walio na itikadi kali.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters

Badala yake Obama ametuma washauri wa kijeshi 300 ambao wameshaanza kukutana na makamanda wa Iraqi tangu jana Jumatano.

Kwengineko Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague amefanya ziara ya kushtukiza mjini Baghdad kuwashinikiza viongozi wa kisiasa wa Iraq kuungana pamoja kukabiliana na wapiganaji hao wa kisuni.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman