1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani kuamua kati ya Trump na Biden

2 Novemba 2020

Nchini Marekani kampeni za uchaguzi wa rais zinaingia siku yake ya mwisho leo Jumatatu ambapo wagombea wote wawili Donald Trump na Joe Biden wako kwenye pilikapilika za lala salama.

https://p.dw.com/p/3klgZ
Kombobild | Donald Trump und Joe Biden

Kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Marekani kimeshakaribia na kimeisogeza ukingoni kabisa nchi hiyo inayokabiliwa na janga kubwa la maambukizi ya virusi vya Corona.

Lakini wakati kampini zinafikia mwisho wake leo na wapiga kura kupata nafasi ya kufanya maamuzi yao Jumanne bado kuna masuala yanayoendelea kuulizwa kuhusu ni haraka kiasi gani matokeo ya uchaguzi huo yatajulikana? Masuali haya yanatokana na wingi wa kura zilizopigwa kwa njia ya barua na uwezekano wa changamoto za kisheria.

Na sababu zote hizo sambamba na uwezekano wa kuzuka maandamano ya kudai haki katika masuala ya kijamii, tahadhari za kukabiliana na virusi vya Corona pamoja na kampini inayoendeshwa na rais Trump ya kueneza taarifa za kujenga hofu miongoni mwa Wamarekani ni mambo ambayo kwa pamoja yamesababisha kuwepo wasiwasi juu ya ikiwa vurugu zinaweza kuzuka nchini humo.

Mgombea urais wa chama cha Democratic Joe Biden amesema ''Kitu pekee kinachoweza kuigawa Marekani ni Marekani yenyewe. Na hicho ndicho hasa anachojaribu kukifanya Trump kuanzia mwanzo. Kuigawa Marekani kwa misingi ya rangi, dini, jinsia, na asili ya utaifa. Ni kosa, hivyo sivyo tulivyo.''

Kura za maoni zaonyesha Biden anaongoza

USA I TV-Duell zwischen Donald Trump und Joe Biden
Mgombea Urais wa chama cha Democratic Joe BidenPicha: Brendan Smialowski/AFP

Baadhi ya wafanyabiashara tayari wameshaamua kufunga biashara zao katika baadhi ya miji wakati kote nchini Marekani mazingira ya kisiasa yakisababisha mijadala mikali na hata ikitajwa kwamba kwa baadhi imesababisha migawanyiko ndani ya familia.

Na katika kile ambacho kinaonesha ni kwa jinsi gani Wamarekani wanashauku ya uchaguzi huu na pengine kutiwa hofu na janga la Corona,idadi ya zaidi ya watu milioni 93 tayari wameshapiga kura ya mapema wengine wakipiga kura hiyo kwa njia ya barua na wengine wakijitokeza vituoni kwa mujibu wa taasisi zisizotegemea upande wowote zinazofuatilia uchaguzi huo.

Kura za maoni zilizotangazwa hadi kufikia leo Jumatatu Trump yuko nyuma ya mpinzani wake. Trump anatazamiwa kuendeleza harakati ya kampeini yake kama ilivyoshuhudiwa siku kadhaa zilizopita ambapo anajipanga kuwakusanya wafuasi wake North Carolina,Pennsylvania,Michigan na Wisconcin.

Joe Biden naye atakuweko Pennsylvania,akiwa kwenye mkutano utakaosindikiwa na mwanamuziki Lady Gaga na pia huko Cleveland katika jimbo la Ohio. Juu ya hilo Wademocrats wanaotaka kuipa nguvu kampeini yao na kuzuia yale yaliyojitokeza mwaka 2016 katika majimbo kadhaa, Barack Obama atakuwa katika jimbo la Georgia kabla ya kuelekea huko Miami katika usiku wa kabla ya uchaguzi.

Jana mgombea wa Republican Donald Trump akiwa Georgia alisema anaamini wafuasi wake kwa mara nyingine wataushangaza ulimwengu. Hofu ya kuzuka mivutano usiku wa uchaguzi na baada ya uchaguzi nchini Marekani zimeongezeka baada ya ripoti kusema kwamba rais Donald Trump huenda akajitangaza mshindi kabla hata ya matokeo rasmi.

Tovuti ya habari ya Axios Jumapili ilitangaza kwamba Trump amewaambia watu wake wa karibu kwamba atajitangaza mshindi Jumanne usiku ikiwa matokeo yataonesha anaongoza.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW