1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbappe asema anafurahia kuwa PSG

16 Februari 2022

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe amesema anafurahia kuwa katika klabu ya Paris St Germain, lakini nyota huyo chipukizi bado hajaamua kuhusu mustakabali wake na miamba hao wa Ligue 1 ya Ufaransa

https://p.dw.com/p/4779d
Champions League - Paris St Germain v Real Madrid
Picha: Andy Rowland/imago images

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe amesema anafurahia kuwa katika klabu ya Paris St Germain, lakini nyota huyo chipukizi bado hajaamua kuhusu mustakabali wake na miamba hao wa Ligue 1. Tetesi zinaendelea kusambaa kuhusu uwezekano wa Mbappe kuhamia Real Madrid ya Uhispania.

Mbappe alifunga bao la dakika ya mwisho wakati PSG iliipiku Real Madrid 1 – 0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano kwenye Champions League.

Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 katika klabu ya PSG unakamilika mwishoni mwa msimu huu. "Sijaamua kuhusu mustakabali wangu. Ninaitumikia PSG, mojawapo ya vilabu vikubwa ulimwenguni,” Mbappe aliiambia televisheni ya Movistar baada ya mechi ya Jumanne usiku.

Bao lake lilizusha shangwe na vifijo kutoka kwa mashabiki wa PSG, na Mbappe akaulizwa kama pongezi hizo za Jumanne huenda zikachangia katika uamuzi atakaoufanya.

"Hapana, sijaamua,” alijibu. "Nitatia bidii na kisha tutaona kitakachofanyika msimu ujao.”

PSG ilikataa ofa ya karibu euro milioni 160 kutoka Real Madrid kwa ajili ya kuitafuta sahihi ya Mbappe Agosti mwaka jana, hata ingawa mchezaji huyo alikuwa na chini ya mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake.

Mbappe, ambaye sasa ana mabao 22 na assisti 16 katika mashindano yote katika PSG msimu huu, anatarajiwa na wengi kuhamia Real Madrid kwa uhamisho huru mwishoni mwa msimu huu, baada ya kukataa ofa ya kusaini kandarasi mpya na klabu hiyo ya Paris.

reuters