1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia yako kipindi kigumu

2 Aprili 2015

Wanadiplomasia waandamizi kutoka nchi sita Alhamisi (02.04.2015) wamekuwa katika vikao muhimu na Iran mjini Lausanne, Uswisi kuharakisha kasi ya mazungumzo ya kufikia makubaliano juu ya mpango tata wa nyuklia wa Iran

https://p.dw.com/p/1F28d
Hoteli ya Lausanne Beau Rivage kunakofanyika mazungumzo ya nyuklia ya Iran nchini Uswisi.
Hoteli ya Lausanne Beau Rivage kunakofanyika mazungumzo ya nyuklia ya Iran nchini Uswisi.Picha: Reuters/Brendan Smialowski

Mazungumzo hayo yameanza upya baada ya vikao vya usiku kucha kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na waziri mwenzake wa Iran Mohammed Javad Zarif halikadhalika mikutano mengine miongoni mwa mataifa hayo sita yenye nguvu duniani kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran ambao inadaiwa kwamba unaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia.Iran inakanusha kuwa na utashi wa silaha hizo na inataka kufikia makubaliano ambayo yataiondolea vikwazo vinavyouathiri uchumi wake.

Akielekea kwenye mkutano wake mwenyewe leo hii Zarif amesema mazungumzo hayo yamepiga hatua kubwa lakini bado rasimu inabidi ziandikwe.Amesema kufikia makubaliano hayo mjini Laussane na makubaliano ya mwisho ifikapo Juni 30 itakuwa kazi ngumu.

Zarif amesema tatizo moja ni kuwepo kwa sauti fatauti upande wa pili meza ya mazungumzo ambapo kuna nchi za Marekani, Urusi,China,Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba inawawia vigumu kuwa na uratibu wa pamoja.

Mazungumzo yako wakati mgumu

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea kusota maafisa wawili wa mataifa ya magharibi wamesema wazo la kutaka kuyasitisha kwa ajili ya sikukuu za mapumziko ya pasaka na kuanza tena wiki ijayo limezungumziwa rasmi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Mohammed Javad Zarif mjini Lausanne.
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Mohammed Javad Zarif mjini Lausanne.Picha: Isna

Mmoja wa maafisa hao amesema mazungumzo hayo yako katika wakati mgumu na njia ya kusonga mbele haiko wazi.Maafisa hao wote wawili wamekataa kutaja majina yao kwa vile hawaruhusiwi kuzungumzia hadharani mazungumzo hayo.

Mazungumzo hayo ya karibuni kabisa katika juhudi za kidiplomasia za zaidi ya muongo mmoja kudhibiti nguvu za nyuklia za Iran yaligonga kisiki Alhamisi muda mfupi kabla ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani kutangaza kwamba wataendelea na mazungumzo hayo kwa kuyaongezea muda maradufu kutoka muda wa mwisho wa kukamilisha mazungumzo hapo Machi 31.

Maazimio madhubuti yatakiwa

Wakati pande hizo zikiwa katika juhudi za kufikia makubaliano Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amefuta ziara yake iliopangwa kufanyika nchini Lithuania,Estonia na Latvia. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius pia amerudi mjini humo baada ya kuondoka hapo juzi.

Wajumbe katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran mjini Lausanne.
Wajumbe katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran mjini Lausanne.Picha: Tasnim

Mataifa ya magharibi yanataka mazungumzo hayo ya Laussane yakamilike baada ya kufikiwa kwa maazimio madhubuti ya makubaliano.

Lakini Iran imeyarudisha nyuma mazungumzo hayo kwa kudai itolewe taarifa ya jumla kwa pasipokuwa na ufafanuzi.Hiyo ni fadhaa ya kisiasa kwa serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani ambayo lazima ilifanye bunge la Marekani lililo hasimu lisadiki kwamba imepiga hatua katika mazungumzo hayo ili kwamba wabunge wasiweke vikwazo vipya jambo ambalo linaweza kuyauwa mazungumzo hayo.

Mhariri : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman