Mazungumzo ya Mashariki ya Kati kushindwa?
28 Januari 2014Mwenyewe Kerry ameshaonya kwamba kuvunjika kwa mazungumzo haya, ambayo ameyapigania bila kuchoka kwa miezi sita sasa, kunaweza kupelekea wimbi la tatu la mapambano ya Wapalestina, maarufu kama intifadha.
Kwa upande mwengine, Wapalestina wanasema wako tayari kuhamishia mapambano yao ya kuwa na taifa huru kwenye ardhi iliyotekwa na Israel katika vita vya mwaka 1967 kwenye Mahakama ya ya Kimataifa ya Uhalifu, pindipo mazungumzo haya yakishindwa.
Kinyume chake, Israel ambayo inaonekana kutokujali kwa kuiendeleza hali iliyopo sasa ikichukua hatua kali za kiusalama zilizopindukia mipaka na ikiendelea na utanuzi wake wa makaazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi, inaweza kuchukua hatua zake za upande mmoja kama mazungumzo haya yatashindwa.
Lakini chochote kitakachotokea, pande zote mbili zitakabiliwa na hali ngumu kiuchumi, endapo haziwezi kutafuta njia ya kugawana ardhi ambayo kila upande unadai ni yake.
Matumaini ni madogo
Mwanadiplomasia mmoja wa Kimagharibi aliyepo mjini Tel Aviv, ambaye hakutaka kutajwa jina, anasema ikiwa mazungumzo yatashindwa, isitazamiwe kwamba Wamarekani watarudi kutiwa tena aibu, na kama wakirudi haitakuwa kwa muda mrefu tena.
Ni wanadiplomasia wachache wanaoendelea kutaraji kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ataweza kuwashinda waliovunjika moyo na kufanikisha makubaliano ya angalau kuruhusu mazungumzo yaendelee baada ya muda wa mwisho wa miezi tisa kumalizika hapo tarehe 29 Aprili.
Lakini bado kukiwa na mambo yanayowagawanya sana, Wapalestina na Waisraili wengi wanaamini kuwa mazungumzo haya hayana yanapokwenda. Bado pande hizo mbili hata hazijaonesha ishara ya kukubaliana kwenye masuala ya kimsingi yakiwemo ya mipaka, usalama, haki ya kurejea kwa wakimbizi wa Kipalestina na hadhi ya mji wa Jerusalem hapo baadaye.
Mohamed Shtayyeh, ambaye alijiuzulu kutoka timu ya wawakilishi wa Palestina kwenye mazungumzo mwaka jana, akilalamikia hatua ya Israel kuendelea kutangaza ujenzi mpya wa makaazi ya walowezi katika maeneo wanayoyakalia kwa mabavu, anasema mazungumzo ya sasa yanaelekea kushindwa na hayataongezwa hata kwa siku moja baada ya muda wake wa mwisho kufika hapo tarehe 29 Aprili.
Israel na Palestina zitaumia
Tangu mazungumzo kuanza mwezi Julai mwaka jana, Israel imeshatangaza mipango ya kujenga nyumba 5,349 mpya kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi ambayo Wapalestina wanaitaka kuanzishia taifa lao.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Israel, Lars Faarborg-Andersen, ameonya kwamba utanuzi huu wa ghafla wa makaazi unamaanisha kwamba Israel ndiyo itakayobebeshwa lawama lau mazungumzo yatavunjika.
"Hofu yangu ni kwamba hatua hii itachochea hali ambapo Israel itajikuta ikizidi kutengwa," alisema wiki iliyopita, akiongeza kwamba makaazi hayo hayawapendezi raia wala wanasiasa wa Ulaya.
Mfuko wa pensheni wa Uholanzi umesema mwezi huu kwamba unaondoa fedha zake katika benki tano za Israel kwa sababu ya kushiriki kwao kwenye ujenzi huo wa makaazi ya walowezi.
Waisraili wanahofia kwamba hasira za Umoja wa Ulaya zinaweza kuiumiza biashara inayofikia thamani ya euro bilioni 30 kati ya pande hizo mbili. Balozi wa zamani wa Israel nchini Canada, Alan Baker, anasema na hapa namnukuu: "Halitakuwa jambo la kufurahisha kwetu, kwa sababu watu wa Ulaya wanaonekana kuwa tayari kuilaumu Israel vyovyote viwavyo." Mwisho wa kumnukuu.
Lakini kwa namna hiyo hiyo, Umoja wa Ulaya umewaonya Wapalestina ambao wanaishi kwa kutegemea misaada, kwamba unaweza kupunguza euro bilioni moja unazowapa kila mwaka, kama wataachana na mpango unaopendekezwa na John Kerry.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Josephat Charo