Mauaji ya wakulima wakizungu yaibua mhemko Afrika Kusini
25 Novemba 2017Mamia ya wakulima wakizungu nchini Afrika Kusini wameingia mitaani kuandamana leo Jumamosi 25.11.2017 katika mji wa Pretoria wakiitaka serikali ichukue hatua juu ya wimbi la mauaji yanayoilenga jamii hiyo katika maeneo ya vijijini nchini humo.
Maandamano hayo ni ya karibuni kabisa kufanywa kuhusiana na mauaji ya kiasi wakulima 72 wakizungu hadi kufikia sasa katika kipindi cha mwaka huu kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na kundi la kampeini ya kupinga mauaji hayo la AfriForum.
Ernst Roets ambaye ni miongoni mwa wanachama wa AfriForum anasema kwamba katika kipindi cha miaka sita iliyopita kumekuwepo ongezeko kila mwaka la mashambulizi na mauaji hayo ya wakulima wakizungu.Wengi wa wanachama wa kundi hilo ni watu wanaozungumza lugha ya Afrikaans inayozungumzwa huko Afrika Kusini.
Maandamano yaliyofanyika huku mvua ikinyesha nchini humo yamekwenda hadi majengo ya serikali ya Afrika Kusini huku waandamanaji wakiwa wamebeba mabango yaliyosomeka maandishi ya kupinga mauaji.Baadhi ya mabango yaliandikwa komesha mauaji ya wakulima na mengine yakiandikwa tunaomboleza.
Dirk Hermann aliyesaidia kuandaa maandamano hayo amesema mauaji ya wakulima ni mengi zaidi nchini Afrika Kusini kuliko mauaji ya watu wengine ikiwemo jeshi la polisi. Mnamo tarehe 30 mwezi Oktoba wakulima wakizungu walifanya maandamano makubwa zaidi katika miji ya Capetown,Johannesburg na Pretoria kupinga dhidi ya kile walichokiita mripuko wa vurugu dhidi ya jamii zao. AfroForum linataka hatua madhubuti zakuonekana zichukuliwe na serikali likisema kwamba maandamano ya Jumamosi yanalenga kuionesha serikali ya Afrika Kusini kwamba watu wamechoshwa na matukio ya kushambuliwa wakulima pamoja na suala zima la ukosefu wa usalama.
Kundi hilo kwa ujumla pia linataka kuundwe kitengo maalum cha kuilinda jamii hiyo.Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka nchini Afrika Kusini baada ya wakulima wawili wakizungu waliotuhumiwa kumfungia kwa nguvu mfanyakazi wao wakiafrika kwenye jeneza na kutishia kumuua kwa kumtuhumu kwamba amekuwa akiwaibia kutoka shambani kwao. Ikiwa ni miaka 23 baada ya kumalizika utawala wa wakibaguzi wa wazungu waliowachache bado nchi hiyo imebakia na mizizi ya mgawanyiko wa rangi na ukosefu wa usawa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri :Isaac Gamba