Mattis awasili Iraq
22 Agosti 2017Ziara hiyo ya Mattis ambayo haikutangazwa inafanyika siku chache baada ya vikosi vya Iraq kuanza mashambulizi katika eneo hilo kubwa la mwisho la mapambano la kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, kaskazini mwa nchi hiyo, ambalo limekuwa likidhibitiwa na IS tangu katikati mwa mwaka 2014.
Mattis amewasili Baghdad kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi na maafisa wengine waandamizi pamoja na Massud Barzani, rais wa jimbo linalojitawala la Wakurdi wa Iraq. Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amesema anataka kusaidia kuufanya utawala wa nchi hiyo unajikita zaidi katika kuwasambaratisha kabisa wapiganaji wa jihadi wa kundi la Dola la Kiislamu.
''Mnaona IS imebanwa katikati ya vikosi imara. Kwa sasa lengo letu ni kuwasambaratisha IS ndani ya Iraq, kuurejesha uhuru wa Iraq na uadilifu wa taifa. Siku za IS zinahesabika, ingawa mapambano bado yanaendelea na hayatamalizika hivi karibuni,'' alisema Mattis.
Mattis amesema mazungumzo yake na viongozi wa Iraq yatazingatia zaidi namna ya kusonga mbele, likiwemo suala la kuiondoa Iraq katika mpasuko wa kisiasa baada ya kuungana kwa karibu miaka minne katika kupambana na wapiganaji wa jihadi.
Mattis ambaye jana alikuwa Jordan, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano itakayomfikisha hadi Uturuki na Ukraine, amesema pia atazungumzia kuhusu kujenga upya makaazi ya maelfu ya Wairaq waliokimbia makaazi na miji yao kutokana na mashambulizi, hasa katika mji wa Mosul.
IS waliondolewa Mosul Julai
Vikosi vya Iraq vikisaidiwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani, viliwaondoa wapiganaji wa IS mjini Mosul mwezi Julai baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa miezi tisa.
Jumapili iliyopita, majeshi hayo yalianzisha mashambulizi katika eneo la Tal Afar, ambalo liliwahi kuwa kituo muhimu cha kupeleka mahitaji ya kundi la IS mjini Mosul, kiasi ya kilomita 70 upande wa mashariki na mpaka wa Syria.
Wakati huo huo, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Iraq kufanya juhudi zaidi ili kuwasaidia maelfu ya wanawake na wasichana wanaokabiliwa na vitendo vya ubakaji, unyanyasaji wa kingono na ukiukwaji mwingine unaofanywa na kundi la IS na kuhakikisha kuwa wanapata huduma za matibabu, ulinzi pamoja na haki.
Katika ripoti hiyo iliyotolewa leo, ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI pamoja na ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, wameonya kuwa watoto waliozaliwa kutokana na matumizi ya nguvu ya kingono, wana hatari ya kukabiliwa na ubaguzi na unyanyasaji katika maisha yao yote.
Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein amesema majeraha ya kimwili, kiakili na kihisia yanayosababishwa na IS, yamepindukia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, AP
Mhariri: Josephat Charo