1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Seneti lachaguliwa

24 Julai 2015

Matokeo ya uchaguzi tata wa rais nchini Burundi yamepangwa kutangazwa baadae hii leo huku baraza la Senet likitarajiwa kuchaguliwa pia hii Leo.

https://p.dw.com/p/1G47A
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Burundi Pierre-Claver NdayicariyePicha: DW/K. Tiasou

Matokeo ya uchaguzi tata wa rais nchini Burundi yamepangwa kutangazwa baadae hii leo huku baraza la Senet likitarajiwa kuchaguliwa pia hii leo.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi Céni,matokeo ya uchaguzi wa rais yamepangwa kutolewa saa tisaa jioni."Wawakilishi wa tume za uchaguzi mikoani wameanza kuwasilisha matokeo ya uchaguzi mjini Bujumbura tangu jana" amesema msemaji wa Céni, Prosper Ntahorwamiye aliyeashiria zoezi hilo lingekamilika alfajiri ya leo.

Hakuna idadi rasmi iliyotangazwa hadi sasa.Walioshiriki ni kati ya asili mia 70 na 80-idadi inayolingana na ile ya chaguzi zilizopita,za bunge na madiwani-zilizofanyika juni 29 iliyopita-ameongeza kusema Ntahorwamiye aliyebainisha hayo ni makadirio yanayotokana na habari kutoka mikoani.

Kwa mujibu wa makadirio ya kituo cha radio na televisheni ya Burundi-RTNB,rais Pierre Nkurunziza,ana uhakika wa kushinda moja kwa moja katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Baraza la Senet lachaguliwa leo

Na huku matokeo ya uchaguzi yakisubiriwa,madiwani waliochaguliwa juni 29 iliyopita wanawachagua hii leo wanachama wa baraza jipya la senet.

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza
Rais Pierre Nkurunziza wa BurundiPicha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Ripota wa DW mjini Bujumbura alizungumza na mmojawapo wa maseneta wa baraza linalomaliza mhula wake Gélase Ndabirabe,ambae ni msemaji wa chama tawala cha CNDD-FDD. Anafafanua jukumu la taasisi hiyo kwa kusema:"Maseneta wana jukumu maalum-inamaanisha baraza la Senet lina jukumu maalum na hasa katika kuhakikisha wezani katika taasisi,sio tu kikatiba bali pia kuambatana na makubaliano ya Arusha. "

Itafaa kusema hapa kwamba baraza la senet linalochaguliwa hii leo halijivunii imani ya baadhi ya mashirika ya kiraia.Madiwani waliopewa jukumu la kulichagua baraza hilo la senet,nao wao pia walichaguliwa katika uchaguzi wa juni 29 uliosusiwa na upande wa upinzani.Na zaidi ya hayo upande wa upinzani daima umekuwa ukiiangalia taasisi hiyo kuwa karibu zaidi na serikali.

Marekani na Umoja wa Ulaya zapanga kuichukulia hatua Burundi

Wakati huo huo serikali ya Marekani inapanga kutathmini msaada wake kwa Burundi katika kipindi cha miezi miwili inayokuja.Matamshi hayo yametolewa na balozi wa Marekani mjini Bujumbura,Dawn Liberi.Marekani inaipatia Burundi msaada wenye thamani ya dala milioni 80 kwaajili ya vikosi vyake vya wanajeshi na miradi mengineyo.Balozi wa Marekani mjini Bujumbura ameitaka serikali ya Burundi ipitishe hatua zinazodhamini misingi ya kidemokrasia,iwapokonye silaha wanamgambo na kuondowa vizuwizi vilivyowekewa vyombo vya habari katika wakati ambapo vituo vya radio za kibinafsi vimefungwa.

EU-Außenbeauftragte Federica Mogherini bei den UN in New York
Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Wenig

Sawa na Umoja wa ulaya,Marekani pia ilimtolea wito rais Pierre Nkurunziza asigombee mhula wa tatu madarakani-lakini wiito huo haukuitikwa.

Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya bibi Federica Mogherini amesema mjini Brussels Umoja wa Ulaya unapanga ikilazimika kuwawekea vikwazo wale wote wanaosababisha matumizi ya nguvu ukandamizaji na kuendewa kinyume haki za binaadam au wanaokorifisha juhudi za kupatikana ufumbuzi wa kisiasa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga