1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ndani ya Umoja wa Ulaya

Lillian Urio14 Juni 2005

Viongozi wa Umoja wa Ulaya, wiki hii, watajaribu kuwathibitishia nchi wanaotaka uwanachama kwamba mpango wa upanuzi wa Umoja huo unaendelea vizuri.

https://p.dw.com/p/CHgX
Bendera ya Umoja wa Ulaya
Bendera ya Umoja wa UlayaPicha: AP

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamekiri kuwa tatizo la katiba ya Umoja huo unaleta utata katika mpango wa kuongeza wanachama.

Umoja wa Ulaya, wenye nchi 25 wanachama, unasisitiza kwamba kura ya Ufaransa na Uholanzi ya kupinga katiba ya Umoja huo haizui mpango wa kuzipa nchi yingine uwanachama. Zikiwemo Romania, Bulgaria, Uturuki na baadhi ya nchi zilizo Mashariki mwa Ulaya.

Lakini pigo hilo kutoka Ufaransa na Uholanzi limeacha swali kubwa, kwamba je, kwa wakati huu, Umoja huo unaweza kuendelea na mpango wake wa upanuzi?

Luxembourg ndio inashika kiti cha Urais wa Umoja wa Ulaya katika kipindi hiki. Kutakuwa na mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja huo, katika mji mkuu wa Brussels, wa wiki hii.

Mwanadiplomasia kutoka Luxenburg amekanusha kwamba kuna tatizo na mpango huo wa kuongeza wanachama.

Kauli hizi za kuondoa mashaka zinakuja baada ya suala la mpango wa kuongeza wanachama, kuwa chanzo cha wananchi wa Ufaransa na Uholanzi, kuikataa katiba hiyo kupitia kura ya maoni. Kura hizo zilipigwa mwaka huu, Wafaransa tarehe 29, mwezi Mei, na Waholanzi tarehe moja, mwezi Juni.

Wapiga kura wengi walisema walipinga katiba hiyo kwa sababu hawakubaliani na Uturuki kuungana na Umoja wa Ulaya.

Ukosefu wa ajira ndio sababu nyingine ya Wafaransa kuipinga katiba hiyo. Wanahofu kuwa watapoteza nafasi zao za kazi kwa raia wa nchi za Ulaya kati, zilizojiunga na Umoja huo mwaka jana.

Kwa mujibu wa maafisa husika, kumekuwa na majadiliano makali kama wahusishe suala la mpango wa kuongeza wanachama, katika mkutano wa wiki hii, utakaoanza Alhamisi ijayo.

Wanahofu kwamba kama hawatalizungumzia, inaweza ikawa ishara mbaya kwa nchi ambazo zinataka kujiunga na Umoja huo.

Sasa hivi Romania na Bulgaria, ndio zinazoleta wasiwasi mkubwa. Zilisaini mikataba mwezi wa Aprili na zinategemewa kujiunga mwezi wa Januari, mwaka 2007. Lakini kutokana na matatizo ya mkataba, kuna hisia kwamba kujiunga kwao kucheleweshwe kwa mwaka moja.

Tayari matumaini ya nchi jirani ya Croatia, ya kujiunga na Umoja huo, yamesitishwa. Nchi hii ilitakiwa kuanza mazungmzo na Umoja huo, mwezi wa Machi, ambayo yangepelekea wao kuwa wanachama.

Lakini yameairishwa kutokana na kile Umoja wa Ulaya unasema ni ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa mji mkuu Zagreb, wa kusaidia kumtafuta mshitakiwa muhimu wa makosa ya kivita.

Kwa upande wa Uturuki hatua itakayo fuata ni kutia saini makubaliano mapya ya masuala ya ushuru na wanachama wapya 10, waliojiunga na Umoja huo mwaka jana, ikiwemo nchi ya Cyprus.

Wakati huo huo, wanadiplomasia na wachambuzi wa mambo wanasema kwamba Uturuki inafurahi kuwa suala la wao kujiunga na Umoja huo halitakuwa katika ajenda ya mkutano huo, baada ya matokeo ya kura ya maoni. Matokeo hayo yalionyesha upinzani mkali dhidi ya Uturuki.

Mwanadiplomasia wa uturuki amesema kwamba wanaelewa matatizo yanayaoikumba umoja wa Ulaya baada ya Wafaransa na Waholanzi kuipinga katiba. Na ndio maana hawasumbuki sana kutokuwepo katika ajenda ya mkutano wa wiki hii.