1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoendelea yanahitaji fedha zaidi kupunguza ujoto duniani.

1 Aprili 2008
https://p.dw.com/p/DYch

Bangkok.

Mataifa yanayoendelea katika mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa unaofanyika katika mji mkuu wa Thailand , Bangkok yamesema kuwa yanahitaji fedha zaidi kutoka mataifa yenye viwanda ili kujiondoa kutoka katika chumi zenye kuharibu mazingira na kutoa gesi zaidi ya carbon.

Wajumbe kutoka mataifa masikini zaidi duniani wamesema kuwa hawatatia saini makubaliano ya kupunguza ujoto duniani mwaka 2009 hadi pale watakapopata dola bilioni kadha kila mwaka.

Mkataba huo unalenga katika kubakisha viwango fulani vya utoaji wa gesi ya carbon katika muongo ujao na asilimia 50 ya punguzo ifikapo mwaka 2050.

Jumla ya mataifa 164 yanashiriki katika mkutano huo wa siku tano wiki hii, ambao unajaribu kutafuta njia ya nini kifanyike baada ya mwaka 2012, wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika.

Wanasayansi wametahadharisha kuwa ongezeko la ujoto duniani litaleta hali mbaya ya hewa itakayoleta uharibifu pamoja na kupanda kwa viwango vya bahari, hadi pale ongezeko la gesi zinazoharibu mazingira litakapodhibitiwa katika muda wa miongo miwili ijayo.