Mashirika ya misaada yahimiza kuruhusiwa kuingia Sudan
18 Aprili 2023Mashirika ya Msalaba Mwekundu na lile la Afya Duniani - WHO yamezitaka pande zinazozozana nchini Sudan kuhakikisha shughuli za kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wanaohitaji zinaendelea bila matatizo na kuhakikisha usalama wa wahudumu wakati ambapo idadi ya watu waliokufa kwenye mapigano hayo ikikaribia watu 200.
Soma pia: Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Alessandra Vellucci amesema umoja huo una takriban wafanyakazi 800 wa kimataifa na wafanyakazi 3,200 wa kitaifa nchini Sudan ambao amesema kutokana na hali ya sasa, hawawezi kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Msemaji wa WHO Margaret Harris amesema hospitali nyingi za mjini Khartoum zinazowahudumia raia waliojeruhiwa zimeripoti kukukabiliwa na uhaba wa mahitaji muhimu kama vile damu, vifaa vya matibabu na vitu vinginevyo vya kuokoa maisha.